
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeridhia uamuzi wa uongozi wa Dayosisi ya Dar es Salaam ya Kanisa la Anglikana, kuinyang’anya familia ya askofu mwanzilishi wa kanisa hilo nchini, marehemu = John Thomas Sepeku, zawadi ya shamba la ekari 20, aliyokuwa amepewa.
Kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, ilifunguliwa na mtoto wa Askofu Sepeku, Bernado Sepeku, dhidi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Ombi la familia ya Sepeku lilihusu shamba lililopo Mtoni Buza, ikipinga uamuzi wa Kanisa wa kumweka mwekezaji, Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co. Ltd.
Mbali na shamba hilo, Bernardo aliiomba mahakama iamuru wadaiwa wote, kwa pamoja au mmojammoja, kulipa fidia ya Sh33 milioni kwa hasara ya uharibifu wa mazao yaliyokuwa katika shamba hilo, pamoja na Sh3.72 bilioni kama fidia ya hasara ya kifedha kutokana na uvamizi wa ardhi hiyo.
Vilevile, aliiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa hao kulipa Sh493.65 milioni ikiwa ni faida iliyotarajiwa, ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na kuvuna mazao hayo, pamoja na fidia nyingine za hasara ya jumla kadiri mahakama itakavyoona inafaa.
Hata hivyo, mahakama imeridhia uamuzi wa Dayosisi ya Dar es Salaam kwamba zawadi alizopewa hayati Sepeku ni mali ya Kanisa, ambalo ndilo lenye mamlaka halali ya kuzimiliki na kuzisimamia.
Kwa maana hiyo, mahakama imeamuru zawadi mbili alizopewa hayati Askofu John Sepeku wakati wa kumaliza utumishi wake wa kanisa zirejeshwe chini ya umiliki wa bodi ya kanisa.
Zawadi hizo ni shamba lenye ukubwa wa eka 20 lililopo Mtoni Buza, Wilaya ya Temeke, pamoja na nyumba moja iliyopo eneo la Kichwere, Buguruni, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Katika hukumu hiyo Jaji Arafa Msafiri aliyesikiliza kesi hiyo, amesema mdai ameshindwa kuthibitisha madai yake kuwa shamba hilo lilitolewa kwa uhalali kama zawadi kwa baba yake.
Jaji Msafiri, katika hukumu aliyoitoa Desemba 16, 2025, ambayo nakala yake imepatikana leo Desemba 19, 2025, amekubaliana na hoja za wadaiwa kuwa Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam iliyotoa zawadi hiyo, haikuwa mmiliki wa mali hizo, bali umiliki halali uko chini ya wadhamini.
Hivyo, amesema Sinodi hiyo haikuwa na mamlaka ya kugawa mali hiyo kama zawadi bila kupata ridhaa ya wadhamini husika.
Ameeleza kuwa mlalamikaji aliegemea mihtasari ya vikao vya kamati tendaji na Sinodi ya Dayosisi, vilivyopendekeza na kuazimia Askofu Sepeku apewe mali hiyo kama zawadi, hatua hiyo haimfanyi kuwa mmiliki halali.
Jaji Msafiri amesema kuwa vielelezo vilivyowasilishwa havithibitishi kwamba marehemu Askofu Sepeku alipewa zawadi hiyo kisheria kwa kiwango ambacho yeye au msimamizi wa mirathi yake, wanaweza kudai kumfanya mmiliki.
Badala yake, Jaji Msafiri amebainisha kuwa ushahidi unaonyesha shamba hilo linamilikiwa kisheria na mdaiwa wa kwanza – Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, kwani limesajiliwa kwa jina hilo, na hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa linamilikiwa na Dayosisi ya Dar es Salaam kama mlalamikaji alivyodai.
“Ni mtazamo wa mahakama hii kwamba hakuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kuwa Dayosisi ya Dar es Salaam ilikuwa au ni mmiliki wa mali inayogombaniwa,” amesema Jaji Msafiri
Amesema hata kama Mahakama ingekubali kauli za mashahidi wa mdai kwamba mali hiyo ilikuwa ya Dayosisi ya Dar es Salaam, Dayosisi haikuwa na mamlaka ya mwisho ya kuitoa bila idhini ya wadhamini, hasa ikizingatiwa kuwa mali hiyo imesajiliwa rasmi chini ya eadhamini.
Aidha, Jaji Msafiri amebainisha kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha kwamba baada ya maazimio ya Kamati Tendaji na Sinodi, zawadi hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa maandishi kama ilivyokubaliwa; kumbukumbu za vikao pekee hazitoshi kuthibitisha uhamisho halali wa umiliki kisheria.
Amesisitiza kuwa ingawa nia ya kutoa zawadi ilikuwepo, uhamisho halali wa umiliki haukufanyika.
“Kwa kuwa mlalamikaji si mmiliki halali wa ardhi inayogombaniwa, hawezi kudai kuwepo kwa uvamizi. Mdaiwa wa kwanza ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo,” amehitimisha Jaji Msafiri.
Ilivyokuwa
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa madai, Desemba 8, 1978, Kamati Tendaji ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake ilipendekeza kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi yenye ukubwa wa ekari 20 pamoja na nyumba.
Zawadi hiyo ilikuwa uamuzi wa Dayosisi ya Dar es Salaam kutambua utumishi wake. Pendekezo hilo la kamati hiyo lilipelekwa katika Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, ambayo katika kikao chake cha Machi 8 na 9,1980 iliridhia pendekezo hilo na iliazimia na kumpatia Askofu Sepeku, shamba lililoko Buza wilayani Temeke, na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Hivyo, familia ya Askofu Sepeku imekuwa ikiishi katika nyumba hiyo na kutumia shamba hilo kwa shughuli mbalimbali tangu wakati huo, huku ikiendelea na mchakato wa kupata hatimiliki, ambao ulikuwa bado haujakamilika.
Hata hivyo, miaka 43 baadaye uongozi wa sasa wa dayosisi uliligawa shamba hilo kwa mwekezaji, kampuni hiyo ya Xinrong, ambaye ilidaiwa kortini kuwa alifyeka mazao mbalimbali, akakata miti na kuharibu uwekezaji mwingine wote ambao familia hiyo ilikuwa imeufanya, zikiwemo nyumba mbili za kawaida.
Badala yake mwekezaji huyo alijenga kiwanda na nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni.
Mwaka huo wa 2023 baada ya kubaini kuwa uongozi wa sasa wa dayosisi ulikuwa umeligawa shamba hilo kwa mwekezaji, ndipo Bernado akafungua kesi hiyo.
Hivyo aliiomba mahakama hiyo iamuru utekelezaji mahsusi kwa mdaiwa wa kwanza (wadhamini) ili kutekeleza mchakato wa kuhamisha umiliki wa shamba na nyumba hiyo, kama ilivyokubaliwa na taasisi zao za ndani, yaani Kamati Tendaji na Sinodi ya Dayosisi, kwenda kwenye mirathi ya marehemu Sepeku.
Askofu Sepeku
Askofu Sepeku alikuwa kiongozi mashuhuri wa Kanisa la Anglikana nchini Tanzania, anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa kanisa hilo baada ya uhuru wa Tanzania.
Alizaliwa 1908, alihudumu kwa miaka mingi katika Dayosisi ya Central Tanganyika kuanzia mwaka 1938 hadi 1960, na baadaye akawa Archdeacon wa Magila kuanzia 1960 hadi 1963.
Mwaka 1970, baada ya Kanisa la Afrikaanse Mashariki kugawanyika, Kanisa la Anglikana Tanzania lilianzishwa kama jimbo huru. Sepeku alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa kwanza na Primate wa kanisa hilo na kutangazwa rasmi Machi 5, 1970.
1978, kutokana na magonjwa, alistaafu kama askofu mkuu, lakini aliendelea kuhudumu kama askofu wa Dar es Salaam hadi alipofariki dunia Novemba 1983.
Askofu Sepeku anatambuliwa kama mmoja wa viongozi wa kanisa waliyeiweka Tanzania kwenye ramani ya Kanisa la Anglikana ulimwenguni na kuchangia maendeleo ya kijamii pamoja na ujenzi wa jumuiya thabiti ya Wakristo nchini.
Alikuwa kiongozi mchangamfu, akifanya ziara nyingi kote nchini ili kukuza umoja wa kanisa na kufungua milango kwa Wakristo wa asili wa Tanzania, akijenga maendeleo ya kiroho na kijamii.