SERIKALI mkoani Geita imeelekeza tathimini mpya ifanyike kufanikisha ukamilishaji wa uwanja wa mpira wa miguu katika Manispaa ya Geita ambao umeshindwa kukamilika kwa wakati.

Mkataba wa mradi wa ujenzi wa uwanja huo ulisainiwa Julai 02, 2021 huku gharama za awamu ya kwanza ikiwa ni sh bilioni 2.4 ambazo ni Fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella ametoa taarifa hiyo katika kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) na kueleza tathimini itarahisisha bajeti ya CSR kutoka Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Amesema mhandisi mshauri (consultant) aliyepewa tenda ya kufanya tathimini atapaswa kutoa ripoti yake kwa kulinganisha miradi ya viwanja tofauti sambamba na gharama inayohitajika.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella.

Ametaja miradi ya mfano itakayotumika ni uwanja wa kituo cha michezo cha Shirikisho la Michezo Tanzania (TFF) mkoani Tanga, kituo cha michezo Kigamboni na uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC).

Shigella ameongeza kuwa mhandisi mshauri aliyepewa kazi atatakiwa kutoa tathimini ya eneo la kuchezea, muundo wake pamoja na gharama zote za kukamilisha matengenezo ya eneo hilo.

Amesema kazi ya pili ya mhandisi mshauri ni kubuni muonekano wa jukwaa kuu na majukwa ya watazamaji wapatao 7,000 ili kazi itakayoanza izingatie uhalisia, mahitaji na bajeti iliyopo.

“Dhamira yetu ni kwamba ligi kuu inayokuja (msimu wa 2026/27), kwanza timu yetu ipande ligi kuu, lakini pili uwanja wetu uwe tayari kutumika kwa ajili ya michezo,” amesema Shigella.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *