Chanzo cha picha, US Department of Justice
Muda wa kusoma: Dakika 7
Idara ya haki ya Marekani imetoa nyaraka za awali zinazohusiana na mhalifu wa makosa ya ngono wa Marekani Jeffrey Epstein.
Nyaraka hizo, ambazo ni pamoja na picha, video na faili za uchunguzi, zilitarajiwa sana baada ya bunge la Marekani kupitisha sheria ya kuamuru faili hizo kutolewa kwa ukamilifu ifikapo Ijumaa.
Hata hivyo, wanachama wa Democrats na baadhi ya Republicans walishutumu Idara hiyo ya Haki kwa kukiuka majukumu yake ya kisheria baada ya kusema kuwa haitaweza kutoa hati zote kufikia tarehe iliyotolewa.
Maelezo mengi katika maelfu ya faili hizo pia yamefichwa au kufunikwa kwa rangi nyeusi.
Watu kadhaa maarufu wamejumuishwa kwenye faili hizo za kwanza, akiwemo Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, Andrew Mountbatten-Windsor, na wanamuziki Mick Jagger na Michael Jackson.
Kutajwa au kupigwa picha kwenye faili hizo sio dalili kwamba walikosa. Wengi wa wale waliotambuliwa katika faili hizo zinazohusiana na Epstein wamekanusha makosa yoyote yale.
Picha ya Bill Clinton akiogelea
Chanzo cha picha, US Department of Justice
Picha kadhaa zilizotolewa ni pamoja na za Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.
Picha moja inamuonyesha akiogelea, na nyingine inamuonyesha akiwa amelala chali mikono yake ikiwa nyuma ya kichwa chake kwenye kile kinachoonekana kuwa ni hodhi ya maji moto yaani bath tub.
Clinton alipigwa picha na Epstein mara kadhaa katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, kabla ya Epstein kukamatwa kwa mara ya kwanza. Waathiriwa wa unyanyasaji wa Epstein hawajawahi kumshutumu Clinton kwa makosa, na amekanusha madai ya kufahamu chochote kuhusu kuhusika kwa Epstein na makosa ya kingono.
Msemaji wa Clinton alizungumzia picha hizo mpya, akisema zilipigwa miongo kadhaa iliyopita.
“Wanaweza wakatoa picha nyingi sana zisizoonekana vizuri kama wanavyotaka za zaidi ya miaka 20 nyuma, lakini hii sio kuhusu Bill Clinton. Haijawahi kuwa, na haitakuwa,” Angel Ureña aliandika kwenye mtandao wa kijamii.
“Kuna watu wa aina mbili hapa. Kundi la kwanza halikujua chochote na lilikata uhusiano na Epstein kabla ya uhalifu wake kujulikana. Kundi la pili liliendelea na uhusiano naye hata baada ya hapo.
“Tuko katika kundi la kwanza. Hakuna hatua zozote kutoka kwa watu wa kundi la pili ambazo zitabadilisha hilo.
“Kila mtu, hasa wafuasi wa MAGA (Make America Great Again), wanatarajia majibu, sio lawama.”
Epstein adaiwa kumtambulisha Trump kwa msichana wa miaka 14
Rais wa Marekani Donald Trump pia ametajwa katika awamu hii ya kwanza ya faili zilizotolewa.
Hati za mahakama zinaeleza kwamba Epstein alidaiwa kumtambulisha msichana wa umri wa miaka 14 kwa Trump katika hoteli yake ya Mar-a-Lago huko Florida.
Wakati wa tukio linalodaiwa kufanyika katika miaka ya 1990, Epstein alimgusa Trump kwa kiwiko na “kumuuliza kwa utani”, akimaanisha msichana huyo, “huyu ni mzuri, si ndio?”, hati hiyo inasema.
Trump alitabasamu na kutikisa kichwa kama kukubaliana, kulingana na kesi iliyowasilishwa dhidi ya Epstein na Ghislaine Maxwell mnamo 2020.
Hati hiyo inasema kwamba “wote wawili walicheka” na msichana huyo alihisi kupatwa na wasiwasi, lakini “wakati huo, alikuwa mdogo sana kuelewa ni kwa nini”.
Mwathiriwa anadai kuwa alitayarishwa kwa namna fulani na kunyanyaswa na Epstein kwa miaka mingi.
Katika kesi hiyo mahakamani, mwathiriwa hakutoa mashtaka yoyote dhidi ya Trump.
BBC imewasiliana na Ikulu ya White House kupata kauli yake.
Tukio hilo ni mojawapo ya matukio machache sana ya kutajwa kwa rais Trump katika maelfu ya faili zilizotolewa Ijumaa. Trump anaweza kuonekana kwenye picha kadhaa lakini uhusishwaji wake ni mdogo sana.
Akaunti rasmi ya X ya The Trump War Room inayotumika kwa operesheni za kisiasa za rais, ilichapisha picha za Clinton baada ya kuachiliwa kwa nyaraka hizo.
Katibu wa mawasiliano wa Trump naye alichapisha tena picha za Clinton, akisema “Oh my!”
Hata hivyo, bado kuna kurasa zaidi ambazo zinapaswa kuachiliwa.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Todd Blanche amesema kuwa kurasa “laki kadhaa” za hati hizo bado zinakaguliwa na hazijawekwa wazi bado.
Rais wa Marekani aliwahi kusema kuwa alikuwa rafiki wa Epstein kwa miaka mingi, lakini akasema walikosana mwaka wa 2004, miaka kadhaa kabla ya Epstein kukamatwa kwa mara ya kwanza.
Trump amekana mara kadhaa kosa lolote kuhusiana na Epstein.
Picha yaonekana kumuonyesha Andrew akilalia mapaja ya watu 5
Picha moja kwenye faili zilizotolewa inaonekana kuonyesha Andrew Mountbatten-Windsor akiwa amelalia mapaja ya watu watano ambao nyuso zao zimefichwa.
Ghislaine Maxwell, mshirikishi mwenza wa makosa ya Epstein, anaonekana kwenye picha hiyo akiwa amesimama nyuma yao.
Andrew amekabiliwa na shutuma kwa miaka mingi kuhusu urafiki wake wa zamani na Epstein, ambaye haonekani kwenye picha hiyo.
Mara kwa mara amekanusha makosa yoyote kuhusiana na Epstein, na kusema “hakuona, kushuhudia au kushuku tabia yoyote ya aina ambayo hatimaye ilisababisha kukamatwa kwake na kuhukumiwa”.
Michael Jackson, Diana Ross, Chris Tucker na Mick Jagger
Chanzo cha picha, US Department of Justice
Hati mpya zilizotolewa ni pamoja na picha nyingi zaidi za watu mashuhuri ambazo hazijaonekana katika matoleo ya faili za Epstein ya awali hadi kufikia sasa.
Epstein alifahamiana na watu wengi katika sekta ya burudani, siasa na biashara.
Baadhi ya picha zilizotolewa zinamuonyesha akiwa na mastaa wakubwa wa muziki ambao ni pamoja na Michael Jackson, Mick Jagger na Diana Ross.
Haijulikani ni wapi au lini picha hizo zilipopigwa, au katika muktadha gani. Haijulikani pia ikiwa Epstein alihusishwa na watu hao wote au kama alihudhuria hafla hizo. Picha zilizotolewa hapo awali zimejumuisha picha ambazo Epstein hakuzipiga mwenyewe, kutoka kwa hafla ambazo hakuhudhuria.
Katika moja ya picha mpya zilizotolewa, Epstein amepigwa picha na Michael Jackson ambapo staa huyo amevalia suti naye Epstein amevalia jaketi.
Picha nyingine ya Jackson inamuonyesha akiwa na Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton na Diana Ross. Wanasimama pamoja katika eneo dogo na nyuso zingine zimefichwa kwenye picha hiyo.
Picha nyingine katika maelfu ya faili inamuonyesha gwiji wa Rolling Stones, Jagger akiwa na Clinton na mwanamke ambaye uso wake umefichwa.
Mwigizaji Chris Tucker pia yuko kwenye picha kadhaa. Moja inamuonyesha akiwa amekaa karibu na Clinton kwenye meza ya kulia chakula. Nyingine inamwonyesha kwenye lami ya uwanja wa ndege akiwa na Ghislaine Maxwell, mshirika aliyehukumiwa wa Epstein.
BBC imewasiliana na Jagger, Tucker na Ross ili kupata maoni yao. Clinton hapo awali alikana kufahamu kuhusu kosa la kingono la Epstein, na msemaji wake siku ya Ijumaa alisema ni picha hizo zilipigwa miongo kadhaa iliyopita.
“Hili halimhusu Bill Clinton. Halijawahi kuwa, na halitakuwa,” msemaji huyo alisema.
Picha ya Maxwell katika ofisi ya Downing Street
Picha nyingine iliyojumuishwa katika toleo hilo inamwonyesha Ghislaine Maxwell akipiga picha mbele ya 10 Downing Street, ofisi ya Waziri mkuu wa Uingereza.
Yuko peke yake, na hakuna maelezo ya muktadha yaliyotolewa kuhusu kwa nini alikuwa hapo au wakati picha hiyo ilipopigwa.
Hatujui ni nani alikuwa waziri mkuu wakati picha hiyo ilipopigwa, au Maxwell alikuwa akitembelea Downing Street katika nafasi gani.
Epstein alitishia kuchoma nyumba, aliyemshtaki anasema
Mmoja wa watu wa kwanza kumripoti Epstein amejumuishwa kwenye faili hizo.
Maria Farmer, msanii aliyefanya kazi na Epstein, aliiambia FBI katika ripoti ya 1996 kwamba Epstein alikuwa ameiba picha za kibinafsi alizokuwa amepiga dada zake wenye umri wa miaka 12 na 16.
Alisema katika madai yake kwamba aliamini Epstein aliuza picha hizo kwa wanunuzi, na alisema kwamba alitishia kuchoma nyumba yake ikiwa atamwambia mtu yeyote kuhusu hilo.
Jina lake limefichwa kwenye faili hizo lakini Farmer alithibitisha kuwa taarifa hiyo ni yake.
Anabainisha katika ripoti hiyo kwamba Epstein alimtaka ampigie picha za wasichana wadogo wakiwa kwenye mabwawa ya kuogelea.
“Epstein sasa anatishia [jina limefichwa] kwamba ikiwa atamwambia mtu yeyote kuhusu picha hizo atachoma nyumba yake”, ripoti hiyo inasema.
Farmer alisema anahisi kueleweka baada ya karibu miaka 30.
“Ninahisi kukombolewa,” alisema.
Kurasa laki kadhaa bado hazijatolewa hadharani
Katika hati zilizotolewa Ijumaa, kuna taarifa nyingi ambazo zimefichwa, zikiwemo taarifa za polisi, ripoti za uchunguzi na picha.
Zaidi ya kurasa 100 katika faili moja inayohusiana na uchunguzi wa jopo zimefichwa kabisa.
Maafisa, kwa mujibu wa sheria, waliruhusiwa kuficha taarifa ili kulinda utambulisho wa waathiriwa, au kitu chochote kinachohusiana na uchunguzi wa jinai unaoendelea, lakini walitakiwa kisheria kuelezea sababu za kuchukua hatua hiyo, jambo ambalo bado halijatekelezwa kufikia sasa.
Maelfu ya kurasa zilizotolewa Ijumaa ni sehemu tu ya kile kitakachokuja, kulingana na idara ya haki ya Marekani.
Naibu Mwanasheria Mkuu Todd Blanche alisema idara hiyo ilitoa “kurasa laki kadhaa” siku ya Ijumaa na kwamba kurasa “laki kadhaa zaidi” zitatolewa katika wiki zijazo.
Aliiambia idhaa ya Fox & Friends kwamba idara hiyo ilikuwa ikitathmini kwa makini kila ukurasa ili kuhakikisha “kila mwathirika – jina lake, utambulisho wao, taarifa yao, zinalindwa kabisa kwa kiwango kinachohitajika”. Alisema kwamba huo ni mchakato ambao huchukua muda.
Muda ambao hati za ziada zitatolewa haujulikani, na wabunge wa pande zote mbili wameelezea kusikitishwa na hali hiyo.
Wanachama wa Demokrats akiwemo Ro Khanna wametishia kuchukua hatua dhidi ya maafisa wa idara ya haki, ikiwa ni pamoja na kura ya kutokuwa na imani nao na kuwafungulia mashtaka kwa kuchelewesha hati hizo.
Khanna alishirikiana na mbunge wa chama cha Republican Thomas Massie kulazimisha kura kupigwa kuhusu sheria ya kuweka wazi faili za Epstein, akipuuza wito wa Rais wa Marekani Donald Trump ambaye mwanzoni alitaka chama chake kupiga kura dhidi ya hatua hiyo.
“Utoaji wa mamia ya maelfu ya kurasa za hati haukuzingatia sheria,” alisema kwenye mtandao wa kijamii, akiongeza kwenye video kwamba pamoja na Massie wanatathmini hatua zote ambazo wanaweza kuchukua.