
Mahakama Maalumu ya Pakistan mapema leo Jumamosi imemhukumu Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Imran Khan, na mkewe Bushra Bibi kifungo cha miaka 17 jela, kila mmoja wao, katika kesi ya ufisadi inayohusiana na ununuzi wa vito vya thamani kwa bei ndogo.
Jaji Maalumu, Shahrukh Arjumand ametangaza uamuzi huo baada ya kuendesha vikao 80 katika Gereza la Adiala.
Rana Mudassir Omar, wakili wa familia ya Khan, amesema mahakama imetoa uamuzi huo bila kusikiliza utetezi, akieleza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya Imran Khan na Bushra Bibi inajumuisha faini kubwa kwao.
Kwa upande wake, chama cha Imran Khan (Pakistan Tehreek-e-Insaf) kimepinga uamuzi wa mahakama, kikisema katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii wa X kwamba “kesi iliyofanyika gerezani si huru wala ya haki, bali ni kesi ya kijeshi,” na kimeitaja kama “kesi ya kimaonyesho.”
Mahakama Maalumu ya Pakistan imeeleza kwamba Imran Khan na mkewe, Bushra Bibi wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na kazi ngumu chini ya Sheria ya Adhabu ya Pakistani kwa kukiuka kiapo cha uaminifu, na miaka mingine 7 chini ya sheria za kupambana na rushwa, pamoja na faini ya rupia milioni 16.4 kila mmoja wao.
Kesi hiyo inahusiana na madai ya ununuzi haramu wa seti ya vito vya thamani iliyopokelewa kama zawadi kutoka kwa mwanamfalme wa Saudi Arabia.
Waziri huyo mkuu wa zamani wa Pakistan Khan amekana kufanya kosa lolote katika kesi hizi, ambazo chama chake kinasema zina matamshi na msukumo wa kisiasa.
Khan, mwenye umri wa miaka 73, amekuwa akitumikia vifungo kadhaa gerezani tangu 2023 kwa makosa ya ufisadi na mashtaka mengine ambayo nyota huyo wa zamani wa kriketi na wafuasi wake wanadai yanachochewa kisiasa ili kuharibu suala yake ya kisiasa. Mkewe, Bushra Bibi, pia alihukumiwa kifungo kwa kosa la rushwa na anatumikia kifungo chake katika gereza hilo hilo, lakini hawaruhusiwi kuonana isipokuwa wakati wanafikishwa mahakamani.
Imran Khan aliondolewa madarakani kama Waziri Mkuu wa Pakistan katika kura ya kutokuwa na imani naye Bunge mwezi Aprili 2022.