Katika kura iliyopigwa siku ya Ijumaa, Baraza hilo lilipitisha kwa kauli moja kuiongezea muda MONUSCO wa mwaka mmoja hadi Disemba 2026.
Kikosi hicho cha askazi karibu 12,000 kilitumwa kwa mara ya kwanza nchini Kongo mwaka 2010 kuchukua nafasi ya ujumbe wa kulinda amani uliokuwa na jukumu kubwa zaidi la kulinda raia na usambazaji wa misaada ya kiutu.
Hata hivyo, hata baada ya miaka 15, Wakongomani wengi wanasema MONUSCO haikutoa ulinzi unaohitajika na raia wakati wa mashambulizi ya makundi ya waasi, na mara kadhaa kumefanyika maandamano ya kuipinga MONUSCO.
Upinzani dhidi ya MONUSCO washuhudiwa Lubero
Kwenye wilaya ya Lubero ambako MONUSCO iliifunga kambi yake mwaka 2023, waakazi wake wanapinga jitihada za kikosi hicho kuifungua tena kambi hiyo.
MONUSCO inataka kuanza tena kazi kwenye wilaya hiyo kuvisaidia vikosi vya Kongo na vile vya nchi jirani ya Uganda kupambana na kundi jingine la waasi la Allied Democratic Forces (ADF). Hata hivyo raia wa eneo hilo wamesema hawaitaki MONUSCO.
“Hatuhitaji askari wa Umoja wa Mataifa kuja kupambana na ADF. Kama vikosi vyetu tiifu vinavyofanya kazi na jeshi la Uganda, vikiamua kwa dhati, vinaweza kuutokomeza uasi wa ADF”, amesema Germain Tiro, anayeishi kwenye kitongoji cha Mangurejipa ambaye amebaini siku za karibuni kuhusu mpango wa askari wa MONUSCO kurejea Lubero.
Mwaka 2023, chini ya ombi la serikali ya Kongo, Baraza la Usalama lilipiga kura kukiondoa kikosi cha MONUSCO kwa awamu na kuanza kukabidhi jukumu la ulinzi kwa vikosi vya serikali.
Hatua ya kurefusha muda wa kikosi hicho imechukuliwa katikati ya kuanguka miji muhimu mashariki mwa Kongo chini ya mikono ya waasi wa M23.
Mapema Januari mwaka huu, waasi hao walichukua udhibiti wa miji ya Goma na Bukavu. Na hivi majuzi waliukamata mji mwingine muhimu wa Uvira lakini walilazimika kuanza kujiondoa baada ya shinikizo hasa kutoka Marekani.
Baraza la Usalama yaitaka Rwanda kuondoa vikosi vyake Kongo
Katika kikao cha Baraza la Usalama cha siku ya Ijumaa, chombo hicho kiliinyooshea kidole cha lawama Rwanda, inayoaminika inawaunga mkono waasi wa M23. Baraza hilo limeitaka Rwanda kuondoa vikosi vyake mashariki mwa Kongo na kusitisha ufadhili wake kwa wapiganaji wa M23.
Azimio la kurefusha muda wa MONUSCO na ukosoaji dhidi ya Rwanda vinajiri katika wakati waasi wa M23 wanadai kuwa wameanza kuondoka mji wa Uvira. Hata hivyo serikali ya Kongo imesema kujiondoa huko ni kwa “kiini macho” na kwamba waasi hao bado wamo kwenye mji wa Uvira.
Naibu Balozi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Jennifer Locetta ameliambia Baraza la Usalama kwamba M23 ni sharti waondoke kwenye mji wa Uvira na wawe umbali wa kilometa 75 za mraba kutoka mji huo.
Waasi hao waliukamata mji huo baada ya siku kadhaa za mashambulizi makali waliyoyafanya licha ya mapema mwezi huu kutiwa saini mkataba wa amani kati ya Kongo na Rwanda chini ya usuluhishi wa Marekani.
Mkataba huo haukulijumuisha kundi hilo, ambalo tayari limo kwenye mazungumzo tofauti na serikali ya Kongo na mapema mwaka huu pande hizo mbili zilikwishakubaliana mjini Doha, Qatar kusitisha mapigano.