Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza mamlaka ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO kwa muda wa mwaka mmoja.
MONUSCO, mojawapo ya ujumbe wa muda mrefu zaidi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 2010 ili kuendeleza na kupanua juhudi za Umoja wa Mataifa za Kulinda Amani na kuleta utulivu nchini DRC.
Ilipokea mamlaka baada ya kusitishwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo Monuc, ambayo ilikuwa kazi tangu Novemba 1999.
Kwa sasa kuna karibu wanajeshi 11,000 na polisi waliotumwa kama sehemu ya operesheni hiyo.
Ukomeshwaji wa FDLR na M23
Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi ya M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kuitaka Rwanda kuacha kuwaunga mkono waasi na kuondoa wanajeshi wake.