
Idara ya Mahakama ya Iran imetangaza kuwa ajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) aliyepatikana na hatia ya kuufanyia ujasusi utawala wa Israel, amenyongwa baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria.
Aqil Keshavarz, aliyepatikana na hatia ya kufanya ujasusi na kushirikiana na Israel amenyongwa leo asubuhi baada ya kukamilika mchakato wa kisheria, na baada ya Mahakama ya Juu ya Iran kutoa uthibitisho wa mwisho wa hukumu yake.
Keshavarz alitiwa nguvuni katika msimu wa machipuo mwaka huu wakati wa doria ya usalama ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa kaskazini-magharibi wa Urmia, baada ya maafisa kumuona akipiga picha kwenye makao makuu ya Kitengo cha Jeshi.
Uchunguzi wa awali ulifichua mawasiliano ya Keshavarz kwenye simu yake ya mkononi yenye anwani zilizounganishwa na Israel, ikiwa ni pamoja na jumbe zinazohusiana na mtu aliyetambulika kama “Osher.”
Upekuzi uliofuata katika makazi yake na chumba chake cha hoteli ulifichua hati, maelezo ya siri na anwani zinazohusiana na taasisi za usalama, na hivyo kuimarisha zaidi tuhuma za ujasusi dhidi yake.
Maafisa wa mahakama wa Iran wameeleza kuwa uchunguzi umeonyesha Aqil Keshavarz alikuwa ameanzisha mawasiliano kupitia mtandao na jeshi la Israel na idara za ujasusi za utawala wa Kizayuni ikiwa ni pamoja na Mossad.
Baada ya uchunguzi uliofanyika na kukiri kwa mtuhukumiwa huyo ilibainika kuwa jasusi huyo wa Israel alikuwa amefanya operesheni zaidi ya 200 kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni Israel kabla ya kukamatwa kwake.