Dar es Salaam. 2025 umekuwa mwaka wa hisia mchanganyiko katika burudani. Wakati wengine wakiuaga kwa mafanikio makubwa kutokana na jitihada zao. Lakini kwa baadhi ya familia mambo yalikuwa tofauti kwa kuwapoteza wapendwa wao ambao waliokuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya burudani.

2025 ni mwaka ulioanza vizuri kukiwa na matukio makubwa ya furaha kwa baadhi ya mastaa kufunga ndoa. Lakini hali ilianza kubadilika na kiwanda cha burudani kujikuta kikiingia kwenye majonzi.

Majonzi hayo yalianzia kwa aliyekuwa  mwigizaji Hawa Hussein Ibrahim (Carina), Hashim Lundenga ‘Mratibu wa zamani wa Miss Tanzania’, Omar Seseme ‘Mpiga gitaa TOT’, Raidanus Vitalis ‘Kitundu’, Mandojo pamoja na Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’.

Hawa Ibrahim ‘Carina’ 

Mwigizaji wa filamu nchini, Hawa Hussein Ibrahim (Carina), alifariki dunia Aprili 15, 2025 akiwa nchini India alikoenda kupatiwa matibabu ya tumbo. Taarifa za kifo chake awali zilitolewa na mwandishi wa habari Imelda Mtema ambaye alikuwa mtu wake wa karibu aliyekuwa akisaidia kusimamia matibabu yake.

Awali Hawa aliondoka nchini Februari 24, 2025 kwenda India kupatiwa matibabu baada ya kukamilika kwa taratibu za safari na gharama ya matibabu Sh54 milioni ambazo zilitokana na michango ya serikali na taasisi mbalimbali.

Mwili wa marehemu msanii huyo uliwasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) Aprili 18, 2025 ukitokea nchini India. Hawa ambaye ameacha mtoto mmoja wa kike aitwaye Aisha mwenye umri wa miaka 16, alizikwa Aprili 19,2025 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Utakumbuka Carina alionekana kama Video Queen kwenye wimbo wa ‘Oyoyo’ wa kwake Bob Junior. Lakini pia alicheza kwenye tamthilia ya kwanza ya mwigizaji Jacob Stephen ‘JB’ ya mwaka 2017 hadi 2018 iliyoitwa ‘Kiu ya Kisasi’.

Hashim Lundenga 

Wakati mashabiki wakiendelea kuugulia maumivu ya kumpoteza Hawa, tasnia ilipokea tena pigo jingine kwa kumpoteza Mratibu wa zamani wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga ambaye alifariki dunia Apili 19, 2025 katika Hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa na Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Bosco Majaliwa ambaye aliiambia Mwananchi kuwa mratibu hiyo alifariki dunia baada ya kupata ‘stroke’ na kuugua kwa muda mrefu.

”Ndio, Hashimu Lundenga amefariki kama saa mbili zilizopita katika Hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta hapa. Hashimu ameumwa muda mrefu sana, nafikiri taarifa ya kuumwa kwakwe watu wengi wanayo, alipata ‘stroke’.

“Alilazwa kwenye Hospitali ya Muhimbili alitolewa, alilazwa Mlongazila akatolewa akawa anaendelea kupata kliniki lakini hali ikazidi kuwa mbaya zaidi,” alisema Majaliwa

Lundenga kwa sasa ni marehemu alisimamia mashindano ya urembo Tanzania na kufanya yajulikane na kupata umaarufu. 
Utakumbuka aliachia kijiti cha kusimamia Miss Tanzania 2018 tangu alipoanza kusimamia shindano hilo mwaka 1994, huku akimkabidhi kijiti Basila Mwanukuzi. 

Hashim alizikwa  Aprili 22, 2025 katika makaburi ya familia, Kidatu, mkoani Morogoro.

Omar Seseme ‘Mpiga gitaa TOT’

Baada ya kutulia kwa takribani siku 20 kikombe cha huzuni kiliwakumba wapenzi na mashabiki wa muziki wa zamani, ambapo walimpoteza mpiga gitaa mkongwe nchini, Omar Seseme. Ambaye alifariki dunia Mei 12, 2025 baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya moyo, akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi, msemaji wa bendi ya Sikinde OG, Mwalimu Hassan Libingai, alisema taarifa za kifo cha Seseme zilipatikana majira ya saa 10 jioni Mei 12, 2025, baada ya majirani kuvunja mlango wa chumba chake saa 8 mchana walipobaini kuwa hakuwa ametoka nje tangu asubuhi.

Libingai alieleza kuwa Seseme alianza kuugua tangu mwaka 2022 na kwa muda mrefu alikuwa akifanya maonyesho akiwa amekaa kutokana na kuchoka kwa mwili wake. 

Seseme, alianza kujiunga na kundi la Sikinde OG mwaka 2022 akitokea Supar Kamanyola ya Mwanza, lakini pia alifanya kazi katika bendi kadhaa maarufu zikiwamo Tam Tam, TOT na nyinginezo.

Raidanus Vitalis ‘Kitundu’

Maisha mengine yakaendelea mpaka Juni 24,2025 ambapo mashabiki na tasnia ya burudani ilimpoteza mwigizaji wa Jua Kali Raidanus Vitalis ‘Kitundu’. Taarifa ya kifo chake ilitolewa na mwongozaji wa tamthilia ya Jua Kali Leah Mwendamseka ‘Lamata’ kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baba yake mdogo Kitundu, Matei Anamboka alisema alifariki dunia Jumanne jioni, katika hospitali ya Temeke alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya tumbo na kifua. 

Kitundu alizikwa Juni 26, 2025, katika makaburi ya Wailes, Temeke.

Aidha enzi za uhai wake marehemu Kitundu mbali na kuigiza kwenye Jua Kali alijihusisha na masuala ya Udensa ambapo alifanikiwa kufanya kazi na wasanii wakubwa ndani na nje ya nchi kama vile Vanessa Mdee, Chino Kidd, Sumalee, na wengine wengi.

Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’ 
Wakati Watanzania wakirudi katika hali yao ya kawaida baada ya kukumbana na matatizo, yaliyotokea  Oktoba 29. Mashabiki wa burudani majira ya saa 2 usiku walipokea habari nzito za kifo cha mchekeshaji na mshereheshaji maarufu nchini, Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’, ambaye alifariki dunia, Novemba 16, 2025 mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gallus Hyela Novemba 18, 2025 alithibitisha kuwa baada ya kushirikiana na madaktari kuufanyia uchunguzi mwili wa MC Pilipili ilibainika kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida.

Hivyo wameanza uchunguzi mara moja kubaini waliohusika.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Dodoma, Dk Ernest Ibenzi naye alithibitisha kifo cha Emmanuel Mathias (MC Pilipili).

Ambapo aliweka wazi kuwa Jumapili saa 11 Novemba 16,2025 walipokea mwili wa MC Pilipili ambao ulipelekwa hospitalini hapo na wasamaria wema.

Hata hivyo baadaye ilibainika kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida kwani mwili wake ulikutwa na majeraha
Mwili wa Mc Pilipili ulizikwa katika makaburi ya Kilimo Kwanza jijini Dodoma Novemba 20, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *