
Dar es Salaam. Bondia wa ngumi za kulipwa Jake Paul amelazwa hospitali akihofiwa kuvunjika taya baada ya kushindwa na bondia bingwa wa zamani wa dunia uzani wa juu, Anthony Joshua, katika pambano lao lililofanyika Miami leo Desemba 20,2025.
Mmarekani huyo alidumu kwa raundi sita dhidi ya Joshua, bingwa wa dunia mara mbili wa uzani wa juu, lakini alishindwa kusimama baada ya kuangushwa mara kadhaa ulingoni.
Paul aliangushwa katika raundi ya tano na ya sita, na baadaye katika maelezo yake amesema anaamini taya lake bila shaka imevunjika.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye pia mwana mtandao maarufu YouTuber baada ya pambano hilo hakuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari
Mkuu wa kampuni ya Most Valuable Promotions, Nakisa Bidarian, alithibitisha kuwa Paul amelazwa hospitali kwa uchunguzi zaidi.
“Tunaamini amevunjika taya, lakini yuko sawa,” amesema Bidarian na kuongeza Jack ameoga kisha akaendesha gari mwenyewe hadi hospitalini.
“Kuvunjika taya ni jambo la kawaida katika michezo, hasa ndondi na muda wa kupona ni kati ya wiki nne hadi sita,” amesema.
Paul aliingia katika pambano hilo akiwa chini ya matarajio makubwa (underdog), huku mbinu zake zikionekana kulenga kutumia kasi na miondoko ya miguu ili kukwepa makonde mazito ya Joshua.
Hata hivyo, pambano hilo lilikumbwa na ukosoaji kutokana na tofauti kubwa ya uzani na uzoefu kati ya wapiganaji hao wawili.
“Tutatibu taya iliyovunjika, kisha nitarudi kupigana na wapinzani wa uzani wangu, ninalenga taji la dunia la cruiserweight.
Nitachukua mapumziko kidogo, nimekuwa nikijituma kwa miaka sita mfululizo.” amesema Paul
Pambano hilo linaacha maswali mapya kuhusu mustakabali wa Paul katika ndondi, hasa anapopambana na wapinzani wenye uzani na uzoefu mkubwa zaidi.