Vita kati ya Urusi na Ukraine vimeingia zaidi ya mwaka wa tatu huku mashambulizi ya Israel kwa Palestina na kinachoendelea Sudan vikiwa ni uthibitisho kuwa matumizi ya silaha yanayoendelea kuongezeka duniani.
Hilo linaashiria nini?
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, matumizi ya fedha kwenye eneo la kijeshi na vita yameongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka 2024.
Uchambuzi wa Reuters ambao umeangazia taarifa kutoka taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI) umeonesha kuwa matumizi yamefikia Dola za Marekani Trilioni 2.7 ikiwa ni ongezeko la asilimia 9 kwa ulinganifu wa kuanzia angalau mwaka 1992 huku vita na machafuko katika miaka mitatu ya hivi kwenye maeneo mbalimbali duniani vikiwa chanzo kikuu cha ongezeko hilo.
Hata hivyo kwa sekta ya biashara ya silaha ‘faida ni kubwa na biashara inashamiri’.
Miongoni mwa ‘wachuma fedha’ wakubwa katika kupaa huko kwa matumizi ya kijeshi ni kampuni kubwa 100 za ulinzi (za utengenezaji na muuzaji wa silaha) duniani ambayo kwa mujibu wa utafiti huo zimejikusanyia takribani Dola Bilioni 679 za Marekani kwa mwaka 2024 pekee huku kampuni zilizo katika tano za juu zikikusanya pato la Dola Bilioni 214.
Katika ukuaji huo wa sekta ya ulinzi, Ulaya imeongoza kwa matumizi ya fedha kwa asilimia 17 kati ya mwaka 2023 – 2024.
Ukraine imeongeza matumizi yake kwa asilimia 34 na kufikia Dola Bilioni 67 kwa mwaka 2024 huku Nchi za Mashariki ya Kati zikiongeza matumizi kwa 15% ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.4 kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya vita ya Israel na Hamas.
Unadhani mweleko huu unaashiria nini katika mataifa yenye uchumi mdogo na rasilimali zinazohitajika zaidi duniani?
Je, Afrika itanusurikaje katika mtego wa vita unaozipa faida kubwa kampuni za Amerika na Ulaya
Imeandaliwa na @moseskwindi