
Arusha. Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar amewaagiza makatibu wakuu wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-Tamisemi), kuhakikisha changamoto ya upungufu wa wataalamu wa ununuzi na ugavi, hususan katika ngazi za chini, inapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Amewaagiza makatibu wakuu hao kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) katika kutekeleza maagizo hayo, akisisitiza ni kinyume cha sheria kwa majukumu ya ununuzi na ugavi kutekelezwa na wataalamu wasio na sifa stahiki.
Maagizo hayo yametolewa jana Ijumaa, Desemba 19, 2025 na Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ally Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, wakati akifungua Kongamano la 16 la PSPTB jijini Arusha.
Amesema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya bajeti yote ya Serikali hutumika katika manunuzi ya umma, hivyo kuboreshwa kwa sekta hiyo kutachangia kuongeza tija na ufanisi wa utekelezaji wa shughuli zote za kisekta nchini.
Ameeleza kuwa Serikali, ikitambua umuhimu wa sekta ya ununuzi na ugavi katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, imeweka msisitizo mkubwa katika matumizi ya mfumo wa NeST kupitia sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali, ili kuhakikisha shughuli za ununuzi na ugavi zinatoa mchango unaotarajiwa katika kufikia malengo ya dira hiyo.
“Nimesikia hapa moja ya changamoto kubwa ni utekelezaji wa ununuzi na ugavi ngazi za serikali za mitaa ambapo shughuli hizo zinatekelezwa na watumishi wasio na taaluma ya ununuzi na ugavi kama walimu, wauguzi na madaktari,” amesema.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Waurugenzi wa PSPTB, Jacob Kibona amesema bodi hiyo imeendelea kusimamia kufanyika kwa ukaguzi wa ukidhi wa sheria ya PSPTB kuhakikishs shughuli za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu wenye sifa stahili.
Amesema katika kaguzi hizo wamebaini uwepo wa upungufu wa wataalamu wenye sifa hususani katika Halmashauri za Miji, Wilaya na Manispaa nchini.
“Sanjari na hilo upungufu wa watumishi wenye sifa umesababisha baadhi ya halmashauri kutumia watumishi ambao ni nje ya taaluma ya ununuzi na ugavi kinyume na kifungu cha 11 cha sheria ya PSPTB,” amesema.