
Mabao ya Reece James na Joao Pedro yametosha kuinusuru Chelsea kukumbana na kipigo kwenye Uwanja wa St. James’ Park dhidi ya wenyeji Newcastle United.
Newcastle United ilikuwa ya kwanza kupata mabao mawili ya uongozi yaliyozamishwa na Nick Woltermade.
Bao la kwanza limepatikana katika dakika ya nne akimalizia mpira ambao uligonga nguzo ya pembeni wakati la pili amefunga kwa kumalizia pasi ya Antony Gordon.
Chelsea ilirejea kipindi cha pili ikiwa imebadilika na kuonyesha nia ya kutaka kurudi mchezoni baada ya James kufunga bao la kwanza kwa mpira wa adhabu.
‘The Blues’ iliendelea kusaka bao lingine la kusawazisha ikifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Newcastle hadi dakika ya 66 ambapo mashambulizi yao yalijibu baada ya mshambuliaji, Joao Pedro kufunga bao la kusawazisha.
Mbrazili huyo ambaye amejiunga na Chelsea msimu huu akitokea Brighton, hilo linakuwa bao lake la tano katika michezo 16 ya Ligi Kuu aliyocheza.
Kocha wa Newcastle, Eddie Howe amelalamikia maamuzi ya refa baada ya kudai beki wa Chelsea, Trevoh Chalobah alimchezea vibaya mshambuliaji wake Gordon katika eneo la hatari ambapo walistahili kupewa penalti.
Kuondoka na pointi moja kwenye michezo huu kunaweza kuifanya Chelsea kushuka katika nafasi iliopo ya nne kwani timu kama Sunderland, Manchester United, Liverpool na Crystal Palace zinaweza kuifikia kwa pointi iwapo kama zitapata matokeo ya ushindi katika michezo yao.
Newcastle bado haipo kwenye nafasi nzuri ikiwa imesogea kwa nafasi moja hadi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo lakini bado inaweza kurudi nafasi ya 12 iwapo Tottenham itapata matokeo mazuri dhidi ya Liverpool hapo baadaye.