YAMETIMIA. Simba SC juzi Ijumaa ilimtambulisha Steve Barker kuwa kocha mpya wa kikosi hicho, hatua inayofungua rasmi ukurasa mpya wa benchi la ufundi la timu hiyo, huku mwenyewe akishusha nondo tatu zitakazomuongoza katika majukumu yake mapya.

Uamuzi wa Simba kumkabidhi Barker mikoba ya Dimitar Pantev unakuja katika kipindi ambacho klabu hiyo inapitia presha kubwa ya matokeo, hasa katika mashindano ya kimataifa, ambako imepoteza mechi mbili za kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien ya Mali kwa mabao 2-1 na Petro Atlético ya Angola kwa bao 1-0.

Barker, raia wa Afrika Kusini aliyezaliwa Maseru, Lesotho, anawasili Msimbazi akiwa na wasifu mzito barani Afrika, hasa kutokana na kazi kubwa aliyofanya ndani ya Stellenbosch FC, klabu aliyojenga kutoka kuwa timu ya kati hadi kuwa moja ya klabu zenye heshima Afrika Kusini na inayotambulika barani Afrika kwa kipindi cha takribani miaka tisa aliyokaa hapo.

Kocha huyo anatajwa kama mmoja wa makocha waliobadili sura ya Stellenbosch kupitia nidhamu yao ya kiuchezaji uwanjani, mpangilio mzuri wa kiufundi na falsafa ya soka la kisasa linaloendana na mahitaji ya soka la ushindani barani Afrika.

Hata hivyo, ana mtihani mkubwa ndani ya Simba, timu ambayo inahitaji matokeo mazuri kwa haraka baada ya hivi karibuni kuonekana kupoteza mwelekeo hasa kimataifa ambapo timu hiyo ina hatihati ya kushindwa kufuzu robo fainali michuano ya CAF kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka saba.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa kwao Afrika Kusini, Barker alisema anafahamu ukubwa wa Simba na uzito wa majukumu aliyopewa, akiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuirudisha klabu hiyo kwenye ramani ya mafanikio.

“Tutajenga timu inayoshambulia kwa ujasiri, inayopigania kila mpira na inayowapa fahari mashabiki wake. Hii ni safari mpya na nawahakikishia tutapigana pamoja,” alisema kocha huyo aliyezaliwa Desemba 23, 1967.

Yeye ni mpwa wa aliyekuwa Kocha wa Bafana Bafana, Clive Barker, aliyeiongoza Afrika Kusini kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika mwaka 1996, taji pekee la AFCON kwa taifa hilo hadi leo. Mbali na hilo, Barker pia ni binamu wa mtayarishaji wa filamu, John Barker.

Akizungumza kuhusu uamuzi wake wa kuondoka baada ya karibu miaka tisa ndani ya klabu hiyo, Barker alisema: “Ni uamuzi wenye hisia mchanganyiko, lakini ninaamini muda umefika kwa Stellenbosch kuanza enzi mpya chini ya uongozi mwingine. Naomba klabu iendelee kupata mafanikio siku zijazo.

“Ninaamini kuchukua changamoto mpya na ya kusisimua katika moja ya klabu kubwa barani Afrika, ni hatua muhimu kwa maendeleo yangu binafsi na malengo yangu kama kocha. Nashukuru kuwa muda wangu Stellenbosch imefungua mlango huo.

“Ningependa kuwashukuru watu wote ndani ya klabu kwa mchango wao mkubwa katika safari yangu hapa Stellenbosch. Nitathamini milele kumbukumbu tulizotengeneza pamoja.”

MTIHANI ALIONAO

Simba baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, inakwenda kukabiliana na Esperance ya Tunisia, Januari 23, 2026, kisha Januari 30, 2026. Mechi hizi mbili za ugenini na nyumbani, zimebeba hatma kubwa ya Simba ama kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali au kuishia njiani.

Kwa sasa Simba ambayo haina pointi katika kundi D, ushindi wa mechi hizo mbili utaifanya kufikisha sita ambazo zitaiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ingawa wapinzani wao nao wanahitaji pointi kwani inazo mbili ikishika nafasi ya tatu, vinara ni Petro Atletico na Stade Malien zenye nne ambazo nazo zinakutana zenyewe mechi mbili zijazo.

Mbali na hilo, pia Barker ana kazi ya kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo ukichukuliwa na watani wao Yanga. Mara ya mwisho Simba ilibeba ubingwa wa ligi hiyo 2020-2021 ikinolewa na Didier Gomes. Pia tangu msimu huo, haijabeba taji lingine kubwa la ndani zaidi ya Ngao ya Jamii 2023 na Kombe la Muungano 2024.

Ukiweka kando mataji, Simba inaonekana haichezi soka la kuvutia kiasi cha mashabiki wa timu hiyo kupiga kelele zilizochangia pia Pantev kusitishiwa mkataba wake Desemba 2, 2025 mbali na matokeo mabaya aliyoyapata siku chache kabla ya kuondoka.

SABABU ZA KUMCHAGUA

Barker aliipa Stellenbosch mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa Carling Knockout Cup 2023, taji la kwanza kubwa katika historia ya klabu hiyo, ushindi uliobadili kabisa hadhi yao ndani ya soka la Afrika Kusini.

Pia aliiongoza timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya CAF kwa mara ya kwanza msimu uliopita, jambo lililowavutia wadau wengi wa soka Afrika na kumwweka Barker kwenye rada ya klabu kadhaa kubwa.

Mafanikio hayo ndiyo yaliyomfanya Simba kumuona Barker kama mtu sahihi, hasa baada ya klabu hiyo kuanza kuyumba katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuhitaji mwelekeo mpya wa kiufundi.

MIFUMO NA FALSAFA

Barker anatambulika kama kocha wa soka la kisasa, mfumo wake unalenga mambo makuu manne, umiliki wa mpira na ujenzi wa mashambulizi kuanzia nyuma, kutoa presha ya juu kwa mpinzani (high pressing), kushambulia kwa haraka kutoka nyuma na ni muumini wa kikosi chenye nidhamu nzuri ya kulianda kuanzia mbele kwa wapinzani.

Katika mifumo, Barker hupendelea zaidi 4-3-3 au 4-2-3-1, akibadilika kulingana na mpinzani. Mabeki wa pembeni hupanda kusaidia mashambulizi, huku viungo wake wakifanya kazi kubwa ya kuunganisha safu zote.

Kwa Simba, falsafa hii inaashiria mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, hasa kwa klabu inayojulikana kwa soka la kushambulia, lakini ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya uwiano kati ya mashambulizi na ulinzi katika mechi za CAF.

HISTORIA YAKE CAF

Barker si mgeni kwa Simba. Anakumbukwa zaidi na mashabiki wa wekundu hao baada ya kukutana nao katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na Stellenbosch ilitolewa kwa matokeo ya jumla ya bao 1-0.

Katika mechi hizo, Simba ilionyesha uzoefu wake wa mashindano ya CAF, huku Stellenbosch ikitoa ushindani mkubwa licha ya kuwa ni mara yao ya kwanza kufika hatua hiyo.

Mechi ya kwanza iliyochezwa Zanzibar, Simba ilishinda kwa bao 1-0, marudiano nchini Afrika Kusini wakitoa suluhu.

Wakati huo Simba ilikuwa chini ya Fadlu Davids ambaye kwa sasa ni kocha wa Raja Casablanca ya Morocco na Barker amekuwa akimtaja Fadlu kama kocha anayemheshimu kutokana na kazi kubwa aliyofanya ndani ya Simba.

Msimu huu kabla ya kuondoka Stellenbosch, Barker ameifanya klabu hiyo kuongoza msimamo wa kundi C katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi nne baada ya mechi mbili, kwa upande wa Ligi Kuu Afrika Kusini, ameliacha chama hilo likiwa nafasi ya 14 katika msimamo ikiwa na pointi 12 katika mechi 14. Stellenbosch imefunga mabao 10 na kuruhusu 18.

KOCHA ANAYEAMINI VIJANA

Moja ya sifa kubwa zilizomtofautisha Barker ni imani yake kwa wachezaji chipukizi. Akiwa Stellenbosch, alijenga utamaduni wa kutoa nafasi kwa vijana na kuwapa majukumu makubwa katika timu ya kwanza.

Barker ndiye aliyempa shavu mchezaji wa Kitanzania, Ally Msengi, kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 18, hatua iliyompa uzoefu mkubwa wa soka la ushindani mapema katika maisha yake ya soka.

Falsafa hiyo ya kuibua na kuendeleza vipaji inaendana moja kwa moja na dira ya Simba ya kujenga timu yenye mchanganyiko wa uzoefu na vijana.

TAMKO LA STELLENBOSCH

Mapema jana, Klabu ya Stellenbosch ilitoa tamko ikithibitisha kuwa, Steve Barker amejiuzulu nafasi yake ya Kocha Mkuu ili kuchukua jukumu jipya la kuinoa Simba.

Katika taarifa yao, imeeleza Barker awali alijiunga na Stellenbosch FC kama kocha msaidizi wa Sammy Troughton msimu wa kwanza wa klabu hiyo, kabla ya kuteuliwa kuwa Kocha Mkuu Julai 2017, uteuzi uliosaidia kuiweka Stellenbosch kwenye ramani ya soka la Afrika Kusini.

Chini ya uongozi wake, Barker aliiongoza timu katika mechi 309 kwenye mashindano yote. Aliisaidia Stellenbosch kupanda daraja kwenda Ligi Kuu ya Afrika Kusini baada ya kutwaa ubingwa wa National First Division msimu wa 2018–2019. Pia aliandika historia kwa kuwa timu ya kwanza kushinda mashindano mapya ya Carling Knockout mwaka 2023.

Aidha, Barker aliiongoza Stellenbosch kufika fainali za MTN8 kwa misimu miwili mfululizo mwaka 2024 na 2025, pamoja na kufuzu mara mbili mfululizo kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Stellenbosch FC, Rob Benadie, alimpongeza Barker kwa mchango wake mkubwa akisema: “Mafanikio ya Steve uwanjani yanaonekana wazi, lakini mchango wake katika kujenga utamaduni, utambulisho na viwango vya kitaaluma vya Stellenbosch FC umekuwa wa muhimu sana.

“Kutumikia klabu moja kwa karibu miaka tisa katika soka la kisasa ni ishara ya uaminifu wa kipekee na kujitolea kwa maono ya muda mrefu ya klabu ingawa kuondoka kwake kunafunga sura muhimu katika historia yetu, klabu ipo katika nafasi nzuri ya kuendelea mbele kwa uthabiti.

“Kwa niaba ya Stellenbosch FC, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Steve na familia yake kwa kujitoa kwao. Tunawatakia kila la kheri nchini Tanzania.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *