Leo ni Jumapili 30 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 21 Disemba 2025 Miladia.
Leo tarehe 30 Azar mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya usiku mrefu zaidi wa mwaka ambao hapa nchini Iran unaitwa Shabe Yalda “Usiku wa Yalda.” Usiku huo wa Yalda au Usiku wa Chelleh ndio usiku mrefu zaidi wa mwaka katika nusu ya kaskazini mwa dunia. Usiku huo huwa baina ya kipindi cha kuzama jua tarehe 30 mwezi wa Azar ambayo ni siku ya mwisho ya kipindi cha mapukutiko (Fall) hadi kuchomoza jua katika siku ya kwanza ya mwezi Dei ambayo huwa siku ya kwanza ya kipindi cha baridi kali (Winter). Wairani na mataifa mengine mengi hufanya sherehe maalumu katika usiku huu wa Yalda. Usiku huo katika nusu ya kaskazini mwa dunia husadifiana na mabadiliko ya kimaumbile na tangu wakati huo mchana huanza kuwa mrefu zaidi kuliko usiku.

Siku kama ya leo miaka 650 iliyopita, “Giovanni Boccaccio” mwanafasihi na mwandishi maarufu wa Italia aliaga dunia. Giovanni Boccaccio, alizaliwa mnamo Septemba 8, 1313, karibu na Florence, Italia. Alikuwa na mchango mkubwa katika fani ya fasihi na alifanikiwa kutoa athari yake yak kwanza akiiwa katika rika la ujana.

Katika siku kama ya leo miaka 201 iliyopita alifariki dunia tabibu na mtaalamu wa masuala ya ardhi wa Uingereza, James Parkinson. Alijifunza tiba kwa baba yake na alikuwa wa kwanza kueleza kwamba ugonjwa wa appendix unaweza kusababisha kifo. Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, kulitiwa saini makubaliano baina ya Umoja wa Kisovieti na utawala wa Baath wa Saddam Hussein kwa ajili ya kuitumia silaha za kisasa Iraq wakati wa kujiri vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Kupanuliwa uhusiano wa pande zote baina ya Iraq na Urusi ya zamani wakati wa vita hivyo, kuliandaa uwanja wa Warusi kufuatilia malengo yao mapya katika sera zao za kigeni katika eneo na mkabala na Iran, huku Iraq ikisaidiwa kisiasa na kijeshi na Urusi sambamba na kupatiwa zana za kijeshi pamoja na misaada ya ushauri wa kijeshi.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, watu 270 walipoteza maisha yao baada ya ndege ya abiria ya Marekani kuripuka katika anga ya Lockerbie huko Scotland. Marekani na Uingereza ziliwatuhumu raia wawili wa Libya kuwa ndio waliotega bomu katika ndege hiyo. Kufuatia mashinikizo ya nchi mbili hizo, mwaka 1992, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea vikwazo vya mafuta, anga na kijeshi nchi ya Libya, kwa tuhuma za kuwaficha Walibya hao. Hata hivyo kufuatia makubaliano kati ya Washington na serikali ya Tripoli, mwaka 1999 watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi ambapo baada ya kesi hiyo mmoja kati ya watuhumiwa hao aliachiliwa huru baada ya kutopatikana na hatia, na wa pili alihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Miaka 12 iliyopita katika siku kama ya leo, Ahmed Asmat Abdel-Meguid, Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90. Ahmed Asmat Abdel-Meguid aliyekuwa mwanadiplomasia wa Kimsri alizaliwa mwaka 1923 katika mji wa Alexandria nchini Misri. Aliongoza Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuanzia mwaka 1991-2001. Kabla ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, Ahmed Asmat Abdel-Meguid alikuwa Waziri wa Mashauuri ya Kigeni wa Misri kuanzia 1984 hadi 1991. Aidha mwaka 1985 alishika wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu. Kadhalika Ahmed Asmat Abdel-Meguid aliwahi kuwa balozi wa Misri nchini Ufaransa na mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa.
