
Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, Naibu Mkuu wa Majeshi ya Iran, amesema “Israel” inajaribu kuficha kushindwa vikali katika Vita vya Siku Kumi na Mbili kupitia njia ya kutoa vitisho, propaganda za vyombo vya habari na ujanja wa kisiasa.
Akizungumza na televisheni ya Al Mayadeen ya Lebanon, Ahmad Vahidi ametoa maoni kuhusu ziara ijayo ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, nchini Marekani na vitisho vinavyoendelea kutolewa na Israel dhidi ya Iran, akisema kwamba utawala wa Kizayuni unatumia vita vya kisaikolojia kupotosha ukweli.
Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi amesema “Israel” inataka kuonyesha taswira ambayo haiakisi hali halisi, akiongeza kuwa utawala huo ghasibu unakabiliwa na matatizo makubwa ya ndani na ya kimkakati na umeshindwa kufikia malengo yake katika kuingia vitani na Iran.
Jeneralii Ahmad Vahidi ameongeza kuwa matamshi na propaganda za Israel haziwezi kuwa na tija, akisisitiza kuwa “Israel” inazidi kutengwa na hivyo kushiriki katika majaribio ya kutaka kubakia hai. Amesema Iran inaendelea kufuatilia kwa karibu harakati zote za Israel.