Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa kuimarisha amani na usalama barani Afrika ni jambo muhimu ili kuhakikisha ustawi wa bara hilo na maendeleo endelevu, na ni kipengee muhimu katika kudumisha amani duniani.

Akizungumza katika Mkutano wa 2 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Russia na Afrika katika mji mkuu wa Misri, Cairo, Lavrov ametilia mkazo dhamira ya Russia ya kuzisaidia nchi za Afrika katika suala hilo.

“Tunatilia maanani masuala ya kuimarisha amani na usalama katika bara la Afrika. Hili ni sharti muhimu la kuhakikisha maendeleo endelevu, ustawi wa kijamii na kiuchumi na ni kipengele muhimu katika kudumisha amani duniani,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia.

Lavrov amesema kuwa Moscow inatoa msaada kwa mataifa ya Afrika katika kusafisha migodi na vifaa vya vilipuzi vilivyoboreshwa na inapanua programu za mafunzo ya kitaaluma kwa wanajeshi na watekelezaji sheria.

Ameongeza kuwa, Russia inaamini kuwa kuna umuhimu wa kutekelezwa kivitendo maamuzi yaliyofikiwa katika Mkutano wa pili wa Russia na Afrika na  kuanzisha utaratibu wa kudumu wa mazungumzo kati ya pande mbili katika ngazi ya juu zaidi ili kuratibu juhudi zote katika uga wa usalama.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia aidha amesisitiza kuwa utatuzi endelevu wa migogoro barani Afrika unahitaji kushughulikia vyanzo vyake, “ambavyo vinatokana na kurithi ukoloni wa Magharibi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *