Utawala wa Israel unaonekana kuandaa mazingira ya kudumisha uwepo wake kijeshi katika maeneo makubwa ya Ukanda wa Gaza. Hii ni kwa mujibu wa uchambuzi mpya wa picha za satelaiti ulioweka wazi ujenzi mkubwa, upanuzi wa miundombinu na kuendelea kuharibiwa mali za Wapalestina tangu kutekelezwa mapatano ya usitishaji vita mwezi Oktoba.

Utafiti uliofanywa na Forensic Architecture, kundi la utafiti wa fani mbalimbali na kuchapishwa na kituo cha habari cha Drop Site News siku ya Jumamosi umeonyesha kuwa utawala wa Israel umejenga kwa uchache vituo 13 vya kijeshi ndani ya Gaza tangu usitishaji mapigano ulipoanza kutekelezwa tarehe 10 Oktoba, huku ukiharakisha kupanua na kuimarisha vituo 48 vilivyopo.

Matokeo ya utafiti huo yamebaini kuwa wanajeshi wa Israel hawakuwa tu wanashikilia nafasi za muda, bali wamekuwa wakilihuisha eneo hilo ili walidhibiti kwa muda mrefu.

Watafiti wamebaini kuwa wanajeshi wa Israel kwa sasa wanadhibiti zaidi ya nusu ya Gaza na wameendelea kupanua udhibiti huo kupitia shughuli za ujenzi na ubomoaji.

Kwa mujibu wa kundi la utafiti la Forensic Architecture, utawala wa Kizayuni umepanua miundo mbinu ya barabara inayounganisha vituo vya kijeshi ndani ya Gaza na kambi za Israel, barabara na vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni  nje ya eneo la pwani, na hivyo kuimarisha ushirikiano wa kilojistiki kati ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu huko Gaza na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu. 

Kundi hilo pia limeeleza kuwa upanuzi wa kijeshi unaofanywa na Israel umekuwa ukienda sambamba na uharibifu wa makusudi wa mali za Wapalestina khususan mashariki mwa mji wa Khan Yunis na katika maeneo mengine kusini mwa Gaza ikiwa ni pamoja na Rafah. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *