
Dar es Salaam. Kampuni inayotoa huduma za kifedha kidijitali, Mixx, leo imekabidhi kiasi cha Sh12 milioni kwa Watanzania wanane kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Geita na Morogoro, kupitia droo yake ya pili ya kampeni ya ‘Magifti ya Mixx Pesa’.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwakabidhi fedha hizo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Wateja Maalum – Mixx, Marry Ruta, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya dhamira ya Mixx katika kuwazawadia wateja wake katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na kugusa maisha yao kiuchumi.
“Nawapongeza sana washindi wetu wa droo hii ya pili ya Kampeni yetu ya Magift ya Mixx Pesa. Washindi hawa wameibuka na ushindi kutokana na matumizi ya huduma za Mixx mara kwa mara kama kuweka pesa, kufanya malipo ya Lipa kwa Simu, kununua vifurushi, kuchukua mikopo ya Nivushe Plus na Bustisha. Niendelee kuwasishi wateja wetu kuendelea kufanya miamala mbalimbali ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye droo ya ushindi.
Miongoni mwa washindi, Anuary Mwinyi, Mkazi wa Bunju na kikazi yeye ni dereva alisema kuwa,
“Kampeni hii imekuja wakati sahihi kwangu. Pesa hizi zitanisaidia kutatua changamoto zangu mbalimbali katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka. Namshukuru Mungu kwa ushindi huu. Nitazitumia kuendesha biashara zangu na kushughulikia changamoto zangu, lakini pia sitamsahau mke wangu; nitampa kiasi kidogo kumsaidia katika shughuli zake za kila siku.”
Washindi wengine pia wameshukuru mtandao huo kwa kuwapa fursa ya kunufaika, wakisema zawadi hizo zitawasaidia kujikwamua kiuchumi hasa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kampeni hio ilizinduliwa Desemba 2, 2025 na inatarajiwa kumalizika tarehe 4 Januari 2026, ikiwa na lengo la kuwazawadia wateja wa mtandao huo katika msimu wa sikukuu.