
Kwa nini Wayahudi wa Uingereza wanakabiliwa na mabadiliko makubwa zaidi katika miaka 60?
-
- Author, Aleem Maqbool
- Nafasi, Mhariri Masuala ya Kidini
- Author, Catherine Wyatt
- Nafasi, Mwandishi Masuala ya Kidini
-
Muda wa kusoma: Dakika 9
“Imekuwa miaka miwili migumu sana,” anasema Phil Rosenberg, rais wa Bodi ya Manaibu wa Wayahudi wa Uingereza. “Nadhani utambulisho wetu wa Kiyahudi unazidi kukumbwa na changamoto siku hizi ukizingatia hali ngumu inyotukabili.”
Migogoro katika Mashariki ya Kati, anasema, imekuwa na athari kubwa kwa jamii ya Wayahudi wa Uingereza.
“Mashambulizi ya Oktoba 7 yalihisiwa sana kibinafsi, sio kwa sababu kulikuwa na Wayahudi wa Uingereza ambao waliuawa katika mashambulizi ya awali na watu wenye uhusiano wa Uingereza walishikiliwa mateka. “Na katika vita vilivyofuata, uharibifu huko Gaza ulikuwa wa uchungu sana kutazama. Kisha kulikuwa na vita vilivyozunguka mzozo mzima, na ongezeko kubwa la chuki dhidi ya Wayahudi na kufikia kilele cha mashambulizi mabaya.”
Ufyatuaji wa risasi kwenye Ufukwe wa Bondi wikendi iliyopita, ambao ulilenga jamii ya Wayahudi wakati wa sherehe za Hanukkah, na shambulio la sinagogi la Manchester katika siku takatifu zaidi katika kalenda ya Kiyahudi, Yom Kippur, pamoja na matukio ya Mashariki ya Kati katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kwa pamoja yamekuwa na madhara makubwa kwa Wayahudi wa Uingereza wanaokadiriwa kufikia 300,000.
Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu vita vya 1967 katika eneo la Mashariki ya Kati ni vigumu kufikiria juu ya hatua hiyo ya kutamka kwa jamii ya Wayahudi ya Uingereza, ambayo imeathiri kwa uwazi maisha ya kila siku.
Kumekuwa na mabadiliko ya mtazamo wa wengi kuhusu usalama, na jinsi wanavyohisi kuhusu utangamano katika jamii. Na pamoja na hayo, pia kuna baadhi ya ushahidi kwamba kumekuwa na mabadiliko katika mazungumzo kuhusu Israel – ikiwa ni pamoja na mgawanyiko wa kizazi ambao unaanza kuwa dhahiri kati ya Wayahudi wa Uingereza.
Bila shaka watu wa mitazamo tofauti, lakini haya ndiyo ya mambo ambayo baadhi ya Wayahudi wa Uingereza wanahisi yamebadilisha maisha yao katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Uhalifu wa chuki na chuki dhidi ya Wayahudi
“Kwa kiwango fulani kulikuwa na uwezekano wa marafiki wa Kiyahudi kuwa na uelewa,” anasema Ben Dory, 33, mkaazi wa London. “Nimeishia kupata marafiki zaidi wa Kiyahudi na pia kujihusisha zaidi na jamii ya Wayahudi.”
Pamoja na kuchukua nafasi kubwa katika sinagogi lake pia amekuwa akifanya kampeni dhidi ya chuki dhidi ya Wayahudi. Hilo kwa kiasi fulani limekuja kwa sababu ya mabadiliko makubwa katika jinsi yeye mwenyewe anavyohisi kuwa salama.
“Ninawajua baadhibya Wayahudi ambao, wakati wanaenda kwenye sinagogi, wanaweka kippah (kofia ya kidini) mfukoni mwao hadi watakapofika mlangoni, na kuivua mara tu wanapoondoka.”
Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Kufuatia shambulio la Australia wikendi iliyopita, Ben aliniambia “ameshtuka, lakini hakushangazwa,” akisema kwamba ilifuata mtindo wa “msisimko wa kimataifa wa kupinga Wayahudi”.
“Ni muda mrefu kumekuwa na matukio ambapo mikusanyiko inayohusiana na Israel inatilia shaka usalama. Lakini sasa Wayahudi wanahisi wako chini ya tishio la mara kwa mara, hata katika mikusanyiko isiyo ya kisiasa ya kitamaduni na kidini,” anasema.
Imekuwa zaidi, kile anachokiita “kisiasa,” katika kipindi cha miaka miwili iliyopita – na sauti zaidi na shauku katika msaada wake kwa Israel. Kwa kiasi fulani ni jibu ambalo anasema linasukumwa na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi.
Kulikuwa na uhalifu wa chuki 1,543 uliowalenga kwa Wayahudi nchini Uingereza na Wales kuanzia mwezi Machi 2023, na kuongezeka hadi 3,282 kufikia Machi 2024, kulingana na idara ya Mambo ya Ndani.
Data ya mwaka unaofuata haijakamilika. Lakini Jumuiya ya Usalama wa Jamii, kundi ambalo limefuatilia idadi ya matukio ya chuki nchini Uingereza kwa takribani miaka 40, inasema viwango katika miaka miwili iliyopita ni vya juu zaidi tangu walipoanza kuweka rekodi zao.
“Wayahudi ninaowajua wanafahamu umuhimu wa Israel salama endapo watahitaji kukimbilia huko,” Ben anasema.

Tangu taifa la Israel lilipoundwa kufuatia mauaji ya kimbari, dhana kwamba Israel inahitajika kama “kimbilio salama” imesalia miohoni mwa Wayahudi wengi – na hisia hii imeongezeka kwa sababu ya matukio ya hivi karibuni, kulingana na baadhi ya wale niliozungumza nao.
“Sijawahi kuhofia usalama wangu kama Myahudi kama ninavyojihisi sasa,” anasema Dame Louise Ellman, mbunge wa zamani, “na hali hii ninayopata inamkabili kila mtu ninayezungumza naye katika jamii ya Wayahudi.”
Alijiondoa katika chama cha Labour mnamo 2019 kwa wasiwasi juu ya chuki chamani humo, na kujiunga tena mnamo 2021; yeye pia ni mwenyekiti huru wa pamoja wa Bodi ya Manaibu, chombo kikubwa zaidi kinachowakilisha Wayahudi nchini Uingereza.
Dame Louise aliwahi kuhudhuria sinagogi la Heaton Park huko Manchester Kaskazini. Aliolewa huko na mwanawe Bar Mitzvah ilishikiliwa hapo.
Hapa ndipo shambulio la mwezi Oktoba lilifanyika, ambalo lilisababisha wathiriwa wawili kuuawa na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Uhusiano wake wa karibu na sinagogi ulizidisha mshtuko aliohisi. “Watu wanazidi kuwa na wasiwasi, wanahisi hasira na kujisikia peke yao,” anasema.
“Hii inasikitisha sana.”
Chanzo cha picha, Getty Images
Haya yote, anaelezea, yamemfanya kuwa muungaj mkono shakiki wa Israel. “Ninafahamu vyema kwamba watu kadhaa, hasa vijana, wanalitazama hili kwa njia tofauti, lakini hao ni wachache sana.”
Mmoja wa wale ambao wamefikia uamuzi tofauti sana kuhusu Israel ni Tash Hyman, mkurugenzi wa ukumbi wa michezo wa miaka 33 kutoka London.
Ingawa miaka miwili iliyopita, anaelezea, ilimfanya ajisikie kuwa ameunganishwa zaidi na Uyahudi wake – kwa mfano, ameegemea zaidi katika mila za uanaharakati wa Kiyahudi – hajisikii kuungwa mkono zaidi na Israel.
“Nilikulia katika mazingira ya kidini ambapo Uyahudi wangu ulihusishwa sana na taifa la Israel, lakini kwa kweli nilianza kuhoji hilo,” anasema. “Jambo la msingi kwangu sasa ni kwamba vitendo vya taifa la Israel vinanifanya nijisikie salama kidogo, sio salama zaidi.
“Inanifanya nisiwe salama Uingereza kwa sababu ya kile wanachofanya huko Gaza.” Anapinga wazo kwamba Israel ni “mahali salama” kwa Wayahudi wa Uingereza.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Takriban watu 1,200 waliuawa wakati Hamas iliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba 2023 na zaidi ya watu 250 walichukuliwa mateka. Tangu wakati huo, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 70,000 wameuawa na hatua za kijeshi za Israel.
Tash anasema kwamba kwa sababu baadhi ya Wayahudi wanaamini kwamba wanaunga mkono vitendo vya Israeli, ni muhimu kwamba wale ambao hawaelezi wazi kwamba kuna upinzani kwa kile ambacho Israeli inafanya kutoka ndani ya jumuiya ya Wayahudi.
Leo anahudhuria sinagogi lakini amezungukwa na wale ambao wana nia moja ya kisiasa – akionyesha kwamba mashambulizi ya Hamas na vita huko Gaza yamefanya mjadala mkali kati ya Wayahudi wa Uingereza kuhusu Israeli kuwa mgumu zaidi.
“Hakika inahisi kama kuna mgawanyiko na hakuna uwezo wa kweli wa kuwa na mazungumzo katika sehemu zote, kwa sababu mgawanyiko ni mkubwa sana.”
Uzayuni: mgawanyiko wa kizazi
Takwimu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Sera ya Kiyahudi (JPR), taasisi ya wataalam ya Uingereza, iliyokusanywa kabla ya shambulio la Manchester na kuchapishwa mwezi Oktoba, zinaonyesha kuwa kuna mgawanyiko wa vizazi kati ya Wayahudi wa Uingereza linapokuja suala la mitazamo kuhusu Israel.
Utafiti uliyojumuisha Wayahudi 4,822 wa Uingereza walio na umri wa zaidi ya miaka 16 ulibaini kuwa idadi ya jumla iliyojitambulisha kama “Wazayuni” ilikuwa 64%, lakini kati ya kikundi cha umri wa miaka 20-30, ni 47% tu ndio waliofanya. Wakati huo huo 20% ya kundi hilo la umri walisema wa “wasio Wazayuni” na 24% kama “wapnga Uzayuni”. (Iliachwa kwa wahojiwa kuamua jinsi ya kutafsiri lebo hizo.)
Idadi ya Wayahudi wanaojitambulisha kuwa wapinga Uzayuni tangu mwaka 2022 imeongezeka katika makundi yote ya rika moja lakini hali kadhalika na pengo kati ya makundi ya wazee na vijana. Kwa mfano, 3% ya wazee wenye umri wa miaka 50-59 waliohojiwa mwaka 2022 walisema wanapinga Uzayuni, pengo la pointi 10 ikilinganishwa na kundi la vijana wenye umri wa miaka 20-29.
Kufikia 2024, ilikuwa ni pengo la pointi 17 – huku 7% ya wazee wenye umri wa miaka 50-59 wakisema kuwa wanapinga Uzayuni, ikilinganishwa na 24% kwa kundi la vijana. (Takwimu zinazolinganishwa kwa umri hazipatikani.)
Chanzo cha picha, AFP via Getty Image
Robert Cohen, ambaue anasomea Shahada ya Uzamivu katika Chuo cha King’s College London, amefanya utafiti wake binafsi kuhusu Wayahudi nchini Uingereza ambao wanakosoa vitendo vya Israel huko Gaza, na nini kiliwafanya kufikia hatua hiyo.
Kati ya Februari 2023 na Oktoba 2024, aliwahoji watu 21 waliochukua msimamo huo na amejaribu kuangazia kwa nini pengo la vizazi huenda linafunguka.
Anaamini kwamba kwa baadhi ya vijana, msimamo wao ulitokana na kile alichokitaja kuwa “maadili ya Kiyahudi ya Uingereza” kuhusu masuala kama vile haki na busara ya kuja pamoja na “Busara ya Gen Z”.
“Tunajua vijana wa kizazi cha Gen Z wana sifa ya uhalisi, kuwa mjumuisho wa hali ya juu, kuwa mkubwa sana katika masuala ya haki,” anahoji. “Na niliweza kuona miongoni mwa kundi langu la utafiti kulikuwa na kuunganishwa kwa mambo hayo na maadili ya malezi yao ya Kiyahudi.”
Wengine niliozungumza nao, ikiwa ni pamoja na Ben Dory, walisema mgawanyiko wa vizazi kuhusu sera ya Israel unaweza kuhusishwa na vijana kuwa na uhusiano mdogo wa moja kwa moja na mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi na ukosefu wa ufahamu wa athari zake.
Chanzo cha picha, Getty Images
Robert Cohen pia anasema wale Wayahudi wa Uingereza aliowahoji ambao wanapinga vitendo vya Israeli huko Gaza mara nyingi walitaka kufanya hivyo pamoja na watu kutoka kwa jumuiya ambazo zinewaelewa zaidi, akimaanisha “kambi ya Kiyahudi” katika maandamano ya Wapalestina.
Pia alizungumzia juu madai ya baadhi ya watu kutokuhurumia mashambulizi ya Hamas.
“Baadhi walisikitishwa na hali ya kutojali kabisa ya madhila wanayopitia waathiriwa wa Kiyahudi wa Israeli kwa kile kilichotokea tarehe 7 Oktoba.”
Kwa kuchukua msimamo uliowachambua Waisraeli, wengi wa wale aliozungumza nao walikuwa wamekosana na marafiki au familia.
Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita vijana zaidi wa Kiyahudi nchini Uingereza walianza kuunga mkono Israel kwa dhati, na hatua hiyo inaweza kuwa na athari kwa uhusiano wa na wale walio karibu nao.
‘Marafiki wangu walinitenga’
Lavona Zarum alizaliwa Israel na kukulia London. Wakati wa shambulio la Oktoba 7, alikuwa mwanafunzi na alikuwa ameteuliwa kuwa rais wa Jumuiya ya Wayahudi katika Chuo Kikuu cha Aberdeen.
“Watu kadhaa walijionda,” anakumbuka. “Nilikuwa na kundi kubwa la marafiki wa kike, lakini mmoja baada ya mwingine walinitenga majira ya joto.”
Anakumbuka jinsi alivyojihisi kutengwa – na jinsi alivyopata ugumu kuzungumza na wanafunzi wengi wasio Wayahudi kuhusu jinsi alivyohisi kuhusu mashambulizi katika Israeli na vita vilivyofuata.
Pia alikerwa na baadhi ya machapisho kwenye mitandao ya kijamii na watu aliowafahamu – mengine yalikuwa kuhusu “kueneza intifadha”.
“Watu walikuwa huru sana kusema wanachotaka, na nilikuwa mwangalifu sana kutoangazia hilo kwa kweli. Nilijitenga moyoni mwangu.”
Chanzo cha picha, PA Media
Lavona ana miaka 21 sasa. Tangu wakati huo amekuwa na uhusiano na marafiki ambao anahisi wanaheshimiana, hata kama hawakubaliani.
Pia alizuru Israel miezi sita baada ya tarehe 7 Oktoba kupitia ushirika na Umoja wa Wanafunzi wa Kiyahudi, akitembelea baadhi ya maeneo yaliyoshambuliwa na Hamas ambapo alisema watu “walizungumza kuwa heshima na kubadilishana mawazo” licha ya kutofautiana kwa maoni.
“Ulimwengu ulikuwa na chuki zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali,” anaongeza. “Lakini imenifundisha kushiriki katika mijadala nikiwa na nia na mawazo zaidi, na pia kujieleza ninapohisi haja ya kufanya hivyo bila hofu.”
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi