Chanzo cha picha, Mahad Mohamud
-
- Author, Bushra Mohamed
- Nafasi, BBC
-
Muda wa kusoma: Dakika 5
Mahad Mohamud 36 anaanza kuzoea polepole joto, machafuko na mivutano katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, baada ya kufukuzwa kutoka jiji la Minneapolis, Marekani mwezi uliopita wakati majira ya baridi.
Wasomali wanamjua kama Garyaqaan, jina analotumia TikTok, ambapo ana wafuasi karibu nusu milioni tangu alipokuwa nje ya nchi.
Lakini kwa wale wanaoendesha akaunti ya “Rapid Response 47” X ya Ikulu ya Marekani, Mahad alikuwa “mhamiaji haramu.” Katika chapisho la mwezi Oktoba akaunti hiyo ilimtuhumu “kuhusika katika utekaji nyara wa maafisa wa Ufaransa” katika hoteli katika mji mkuu wa Somalia.
Mahad amekanusha madai hayo, akisema hakuwa Mogadishu wakati huo. Hakuwahi kuhukumiwa na kesi hiyo ilifutwa.
Anasema kukamatwa kwake na shirika la Uhamiaji na Forodha la Marekani (ICE) kulisababishwa na mpinzani wake TikToker kuvujisha anwani yake.
“ICE iliniambia walikuwa na kesi mbili dhidi yangu – moja ilikuwa kuingia nchini kinyume cha sheria na utekaji nyara wa afisa wa Ufaransa.”
Mahad alisema kesi ya utekaji nyara ilishughulikiwa na FBI na baada ya kuhojiwa, walimkuta hana hatia.
Lakini hilo halikumwokoa kutokana na kufukuzwa.
Safari yake kutoka Somalia hadi Marekani ilianza zaidi ya muongo mmoja uliopita na ilimpeleka kwanza Afrika Kusini, ambapo aliishi hadi 2021. Lakini anasema alishambuliwa na watu wenye silaha katika shambulio la chuki dhidi ya wageni.
Kisha akaenda Brazil , hatimaye akavuka hadi Marekani, bila hati miliki, kupitia mpaka wa Mexico.
“Nilipoingia kutoka Mexico, nilikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja,” anasema Mahad.
“Baadaye niliachiliwa na kupewa kibali cha kazi kwa sababu kesi yangu ya kuomba hifadhi ilikuwa bado iko wazi.”
Kisha akaelekea Minneapolis. “Nilikuwa nikifanya kazi kama dereva wa Uber. Nilifurahi kuwa katika nchi ya ndoto yangu.”
Video zake za TikTok pia zilimpa mapato huku mashabiki wakimtumia zawadi walipokuwa wakitazama matangazo yake ya moja kwa moja. Pia ilisababisha tishio kwa maisha yake kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab lenye makao yake Somalia kwa sababu ya kuitetea serikali.
Sehemu ya kesi yake ya kuomba hifadhi nchini Marekani ilitokana na tishio hilo.
Kukamatwa na kufukuzwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Mahad anaelezea kwa undani asubuhi moja ya Mei mwaka huu, maafisa wa uhamiaji walipomkamata.
Kulingana na Mahad, alichukuliwa kwa gari kwa dakika 30 hadi makao makuu ya ICE, Minneapolis, kabla ya kuhamishwa kwa safari ya saa sita hadi Gereza la Kaunti ya Kandiyohi huko Willmar, Minnesota, ambapo anasema alikaa miezi sita kizuizini.
Anaiambia BBC miezi mitatu kati ya hiyo ilitumika kusubiri uamuzi kuhusu kesi yake ya kuomba hifadhi, na miezi mitatu iliyobaki ikisubiri kufukuzwa. Mamlaka ilikataa dai lake la kuomba hifadhi kwani madai kwamba atakuwa hatarini nchini Somalia yalikataliwa.
Hatimaye, ilipofikia siku ya kuondoka, Mahad anasema alivaa koti na kusafiri kwa ndege ndogo akiwa na wahamiaji wengine saba na baadhi ya walinzi.
Safari hiyo iliwapeleka kwanza Costa Rica, Amerika ya Kati, kisha Senegal huko Afrika Magharibi, kabla ya kuruka hadi mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Huko Mahad anasema koti liliondolewa na akafungwa pingu na kuwekwa kwenye ndege nyingine hadi Mogadishu.
Baada ya kukaa miezi mitatu akisubiri kufukuzwa, Mahad alikuwa tayari amekubaliana na hatima yake, hakuhuzunika aliporudi.
Baada ya muongo mmoja, hatimaye ameungana tena na watoto wake watatu. “Sijawaona kwa miaka 10,” Mahad anasema.
Lakini bado anapendelea kuwa Marekani kwa sababu anahofia maisha yake baada ya kupokea jumbe za maandishi kutoka kwa al-Shabab, zenye vitisho vya kifo.
Anachukua tahadhari zaidi za usalama anapokuwa nje na anaishi katika nyumba inayolindwa vizuri.
Aliporudi, Mahad alikaribishwa na watu wengi kutoka ukoo wake, wakiwemo wanasiasa wa eneo hilo, kwa sababu ya wasifu wake TikTok.
Anaelewa kwamba kwa sababu ya uwepo wake kwenye mitandao ya kijamii anaweza kupata fursa ambazo hazipatikani kwa Wasomali wengine waliofukuzwa.
Sera za Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi uliopita, Rais Donald Trump alisema atasitisha hadhi ya kutoa ulinzi ambayo inazuia watu kufukuzwa Marekani ikiwa nchi zao sio salama.
Mapema mwezi huu, alisisitiza kwamba hataki wahamiaji wa Somalia nchini Marekani, akiwaambia waandishi wa habari kwamba wanapaswa “kurudi walikotoka.”
Somalia haijawa na serikali ambayo inadhibiti nchi nzima tangu kupinduliwa kwa Rais Siad Barre mwaka 1991. Watu wamelazimika kuvumilia miaka mingi ya machafuko na ukosefu wa usalama – na hata sasa, licha ya serikali kuwepo Mogadishu, wanamgambo wa Kiislamu bado wanatawala sehemu kubwa ya nchi na mara kwa mara hufanya mashambulizi katika mji mkuu.
Matamshi ya Trump yalikuja baada ya kuulizwa kuhusu ubadhirifu mkubwa wa pesa katika mpango wa usaidizi wa kijamii wa jimbo la Minnesota.
Watu kadhaa wameshtakiwa na waendesha mashtaka wa shirikisho wanasema ulihusisha shirika la kutoa misaada kuitoza serikali ya jimbo hilo bili ya chakula kwa watoto wakati wa janga la Covid-19.
Wahamiaji kadhaa wa Somalia wanahusishwa na ubadhirifu huo.
Kufuatia matamshi ya rais kuhusu Wasomali, video zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionekana kuonyesha maafisa wa uhamiaji wakigonga milango kote Minneapolis, ikijumuisha eneo linalojulikana kama Little Mogadishu, na St Paul.
Kwa wengi katika jamii ya Wasomali jijini humo, ambayo ni kubwa zaidi nchini Marekani – ikiwa na takriban watu 80,000, matamshi hayo yamezua wasiwasi.
Mahad si peke yake aliyefukuzwa Somalia katika miezi ya hivi karibuni, ingawa hakuna takwimu rasmi.