
Wapalestina wawili, akiwemo kijana mmoja, wameuawa shahidi huku wengine wawili wakijeruhiwa kwa risasi baada ya vikosi vya Israel kufanya mashambulizi tofauti katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ghasia za hivi punde dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.
Shirika rasmi la habari la Palestina WAFA, likinukuu Wizara ya Afya, limeripoti kuwa Rayyan Mohammad Abu Mualla aliyekuwa umri wa miaka 16 alipoteza maisha yake kutokana na risasi za Israel katika mji wa Qabatiya, kusini magharibi mwa Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi. Wizara hiyo imeongeza kuwa, mwili wa mwathiriwa unazuiliwa na wanajeshi wa Kizayuni.
Picha za video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha kijana huyo akitembea njiani, mara ghafla akafyatuliwa risasi na wanajeshi makatili wa Israel.
Mapema jana, Mpalestina mwingine kwa jina Ahmad Saed Shahada Zeyoud, aliyekuwa mwenye umri wa miaka 22 pia aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi kifuani na wanajeshi wa Israel walipovamia mji wa Silat al-Harithiya, magharibi mwa Jenin.
Kadhalika Mpalestina mwingine mmoja ameuawa shahidi na jeshi la Israel huko Gaza katika ukiukaji wake wa hivi punde wa usitishaji mapigano ulioanza kutekelezwa mwezi Oktoba. Haya yanajiri siku moja baada ya Wapalestina wengine 5 kuuawa shahidi Gaza.
Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na mashambulizi makali ya kijeshi ya Israel na kuongezeka kwa vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa walowezi tangu vita vikali huko Gaza, ambavyo vimeua zaidi ya watu 70,000 katika eneo hilo la pwani, kuanzia Oktoba 2023 hadi sasa.
Zaidi ya Wapalestina 1,102 wameuawa shahidi tangu wakati huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na wengine zaidi ya11,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya wanajeshi na walowezi wa Israel katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu. Takriban Wapalestina 21,000 pia wametekwa nyara na vikosi vya utawala ghasibu wa Israel.