
Uchunguzi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC umefichua kashfa ya utapeli, ambapo Muisraeli amekuwa akipokea misaada eti kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wa saratani nchini Canada.
Katika uchunguzi huo, shirika la BBC liligundua kuwa, kashfa hiyo ya kimataifa ya taasisi moja ya Mzayuni kupokea misaada kwa ajili ya wagonjwa wa saratani iliwanyanyasa watoto wanaosumbuliwa kweli na maradhi hayo, na familia zao.
Erez Hadari, mwanammme wa Kiisraeli anayeendesha taasisi ya Walls of Hope nchini Canada, alichangisha mamilioni ya dola katika michango ambayo haikuwafikia watoto ambao walipaswa kuwasaidia. Licha ya kukusanya karibu dola milioni 4 katika kampeni hiyo, BBC imezungumza angalau na familia tisa ambazo hazijapokea chochote.
Wazazi walisema walidanganywa, walidaiwa, na kuachwa bila usaidizi huku watoto wao wakipambana na makali ya saratani. Kampeni za uchangishaji fedha ziliendeshwa na mtandao unaohusishwa na mwanamume huyo wa Israel anayeishi Canada.
Hadari anahusishwa na mashirika kadhaa ya kutoa misaada yenye makao yake makuu nchini Marekani na Israel, ikiwa ni pamoja na taasisi ya “Chance Letikva,” ambayo pia inajulikana kama “Chance for Hope.”
Uchunguzi wa BBC uligundua kuwa, Hadari aliajiri maskauti kutafuta watoto warembo wenye umri wa miaka mitatu hadi tisa. Maskauti hao waliambiwa waende kwenye kliniki za saratani na kuangazia watoto wenye vipara wenye saratani na wakawataja kuwa “wazuri.”
Watoto hao wagonjwa, ambao walikuwa wametoka nchi mbalimbali, walitumiwa katika video zenye hisia, wakiomba msaada na kudai maisha yao yalikuwa hatarini.
Wakati wa upigaji picha, uchunguzi wa BBC uligundua kuwa baadhi ya watoto hao walikuwa wameunganishwa na vifaa vya matibabu ghushi, huku maskauti wakitumia vitunguu vilivyokatwakatwa na ‘menthol’ ili kufanya watoke machozi, waonekane kana kwamba wanalia kwa maumivu.