UONGOZI wa TMA unatarajia kukutana wiki hii na kocha wa kikosi hicho, Habibu Kondo ili kuzungumzia mambo mbalimbali ya timu hiyo, hususani wachezaji wa kuwaongeza katika dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa kuanzia Januari Mosi, 2026.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa TMA, Chris Salongo, amesema watakutana na kuzungumza na benchi la ufundi la timu hiyo kwa ajili ya kusikiliza mapendekezo yao ya wachezaji wanaowahitaji, kutokana na upungufu waliouona hadi sasa.

“Sisi kama viongozi tuna mapendekezo yetu kutokana na vile tulivyoona ila, tutawasikiliza na kuona wao pia wameona nini, lengo kuu ni kutengeneza kikosi cha ushindani kwa sababu gepu la pointi na washindani wetu sio kubwa,” amesema Salongo.

Aidha, Salongo amesema licha ya malengo makubwa ya kuboresha kikosi hicho, ila watazingatia balansi katika maeneo yote muhimu uwanjani, ambapo baada ya kukaa na benchi la ufundi wataunda mikakati mizuri ili wasivuruge na kuanza tena upya.

Timu hiyo ya jijini Arusha, imecheza mechi 11 za Championship, ikishinda mitatu, sare mitatu na kupoteza mitano, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao sita huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane, ikiwa nafasi ya 11 na pointi 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *