INDIA; Serikali ya Tanzania na India zimesaini Hati ya Makubaliano kuhusu ushirikiano kwenye Sekta ya Afya katika kuendeleza tiba asilia (Ayurveda).

Aidha, Tanzania imewakaribisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuwekeza na kuwahakikishia kuwapatia mazingira mazuri ya uwekezaji.

Utiwaji saini huo umefanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Bharat Mandapam uliopo New Delhi, India kati ya Waziri wa Afya wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa na Waziri wa Afya anayeshughulikia Tiba Asili (AYUSH) wa India, Jagat Prakash Nadda katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu tiba asilia,.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus aliyeshuhudia utiaji saini huo amepongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa inayofanya katika sekta ya afya na kusisitiza kuwa, WHO litaendelea kushirikiana kikamilifu na Tanzania katika sekta ya afya.

Akifunga mkutano huo uliowashirikisha mawaziri wa afya kutoka zaidi ya nchi 100 na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesisitiza umuhimu wa kulinda haki miliki, maarifa ya jadi pamoja na matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia za kidijiti kuhifadhi, kuthibitisha na kulinda maarifa ya tiba asili.

Aidha, amesema teknolojia haitachukua nafasi ya waganga wa jadi, bali itaongeza na kulinda hekima yao.

Kwa upande wake, Mchengerwa amesema kusainiwa kwa hati hiyo ya makubaliano ni hatua muhimu kwa Tanzania na kwamba, kunaimarisha ushirikiano wa kitaasisi baina ya Tanzania na India katika maeneo ya kipaumbele ya sekta ya afya, kuongeza uwezo wa rasilimali watu katika sekta hiyo, kuimarisha udhibiti na matumizi salama ya tiba asilia pamoja na kuchangia jitihada za serikali kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kufikia Bima ya Afya kwa Wote.

“Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya serikali kupitia Wizara ya Afya katika kukuza tiba asilia salama, yenye ushahidi wa kisayansi na inayosimamiwa kwa misingi madhubuti ya udhibiti, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya afya kwa watu wote,” amesema Mchengerwa.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania inaendelea kubadilisha tiba asili kutoka katika hekima ya kurithiwa kizazi hadi kizazi, na kuifanya kuwa tiba inayothibitishwa kisayansi, inayolindwa kidijitali na yenye uwezo wa kibiashara kwa manufaa ya afya duniani kote.

“Serikali ya Tanzania inaamini kuwa, tiba asilia inapolindwa na sheria huku ikiimarishwa na sayansi, ikawezeshwa na teknolojia na kuendeshwa kwa mtazamo wa kibiashara, inaweza kuwa nguzo muhimu ya kimataifa katika kujenga jamii zenye afya bora,” amesema.

Amesema bado tiba asilia ni muhimili muhimu wa huduma za afya ya msingi Tanzania.

Inasemekana kuwa, takribani asilimia 60 ya Watanzania hutumia huduma za waganga wa tiba asilia, ama kabla au sambamba na huduma za hospitali na kwamba, hali hiyo inaonesha kuwa, upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi si hiari, bali ni lazima.

Mchengerwa amebainisha kuwa, Tanzania imeweka msingi thabiti wa kisheria na kikanuni kupitia Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Namba 23 ya Mwaka 2002 inayotekelezwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Hadi sasa bidhaa 141 za tiba asili zimesajiliwa nchini Tanzania na zaidi ya asilimia 90 huzalishwa na wajasiriamali wadogo wa ndani wakiongozwa na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya.

Nje ya mkutano huo, Mchengerwa amefanya majadilino na wawekezaji kadhaa wa sekta ya dawa ili kuvutia uwekezaji wenye maslahi kwa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *