Umoja wa Afrika AU umetangaza kumuunga mkono Jenerali Abdel Fattah al Burhan na serikali yake nchini Sudan na kusisitizia wajibu wa kurejeshwa umoja wa ardhi na utulivu wa nchi hiyo. Pia umetoa mwito wa kufanyika mazungumzo baina ya pande hasimu ili kukomesha vita vya umwagaji damu visivyo na sababu ya maana.

Mwandishi wa televisheni ya Al-Alam ameripoti kuwa, baada ya kusimamisha shughuli zake kwa muda mrefu, hatimaye Umoja wa Afrika umepeleka ujumbe wa maandishi kutoka kwa mkuu wa umoja huo kupitia Mohamed Belaish ambaye ni mjumbe maalumu wa AU nchini Sudan, ukitilia mkazo wajibu wa kuchungwa mistari myekundu kati ya Sudan na Misri.

Mistari hiyo myekundu ni pamoja na kuhakikisha kwamba umoja wa ardhi ya Sudan unalindwa kikamilifu, kutotenganishwa usalama wa Misri na usalama wa Sudan, kuhakikisha kunafikiwa makubaliano ya pamoja ya ulinzi kati ya nchi hizo mbili, na kutotambuliwa kikosi chochote kilichoko nje ya udhibiti wa serikali ya Jeneral al Burhan.

Belaish amesema: Mashambulio ya kitaasisi dhidi ya raia na mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanywa na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na uharibifu wa miundombinu ya Sudan vyote ni jinai zinazopaswa kulaaniwa kwa maneno makali, na wahusika wa jinai hizo hawatokwepa adhabu.

Umoja wa Afrika umetangaza kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vilifanya mauaji dhidi ya raia katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam, ambayo yalikukwa makubwa kiasi kwamba yamefikia daraja ya jinai za kivita.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Alam, juhudi za kidiplomasia, mashinikizo ya kimataifa na vikwazo dhidi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vimewekwa kutokana na ukiukaji wa mara kwa mara wa haki za binadamu na kuua raia wasio na hatia huko Sudan. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jinai nyingine za RSF ni kushambulia vituo vya huduma za umma huko Sudan.

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vilianza Aprili 15, 2023. Majenerali hao wa kijeshi wanaongoza makundi mawili hasimu ya SAF na RSF na wamesababisha maafa makubwa kwa raia na nchi nzima ya Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *