Dar es Salaam. Wamiliki wa viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula nchini wamelia na biashara ya magendo, huku wakiitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza nguvu katika kuidhibiti.

Wametoa kauli hiyo wakati wakizungumza na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alipofanya ziara kwenye viwanda vya East coast Oils and Fats (Mo), African Harmony (Wilmar) na Mikoani Traders (Azania Company) Desemba 20 mwaka huu.

Kilio cha wafanyabiashara hao kimekuja siku chache tangu TRA ikamate madumu 23,775 ya mafuta ya kupikia yaliyoingizwa  kimagendo kupitia bandari ya Kunduchi jijini Dar es Salaam,  huku madumu 5,000 pekee yakiwa na nyaraka halali.

Kwa mujibu wa TRA madumu 18,255 kati ya 23,755 hayakuwa na nyaraka zilitakiwa kulipiwa kodi ya Sh438.12 milioni ikiwa ni sawa na Sh24,000 kwa kila dumu.

Hata hivyo kutokana na kukutwa na makosa ya kijaribu kukwepa kodi ikiwa mmiliki atataka kuukomboa mzigo wake atalazimika kuongeza fedha zaidi na atakaposhindwa mzigo utataifishwa.

Akizungumza na Kamishna wa TRA, Mkurugenzi wa Utawala Azania Company, Salehe Afif amesema biashara ya mafuta ya magendo imekuwa ikiwaathiri kwa kiwango kikubwa, kwani inafanya bidhaa wanazozalisha kuwa na soko hafifu.

“Viwanda vyetu vimeajiri watumishi wengi na vinatarajia kuwalipa mishahara kupitia uzalishaji na uuzaji, lakini kuingiliwa kwa soko kunatufanya tushindwe kujiendesha vizuri ,” amesema Afif.

Mkuu wa Idara ya rasilimali Watu na Utawala wa Kiwanda cha Wilmar, Gerald Lyimo aliitaka TRA kuendelea kupambana na magendo hayo ili kunusuru viwanda vya ndani vinavyozalisha mafuta.

Mmiliki wa Kiwanda cha East Coast Oils and Fats (MO) kilichopo jijini Dar es Salaam, Gulam Dewji amesema uingizwaji wa mafuta ya magendo haukubaliki kwani unaharibu biashara na kudhoofisha viwanda vya ndani.

“Sisi kama wamiliki wa viwanda vya kutengeneza mafuta tupo tayari kushirikiana na TRA kwani jitihada hizi zinahitaji nguvu ya pamoja,” amesema.

Dewji alitumia nafasi hiyo pia kuonyesha namna anavyoridhishwa na jitihada zinazofanyika katika kuhakikisha mazingira ya biashara kwao yanakuwa sawa.

Akizungumza kiwandani hapo, Mwenda amesema TRA inaendelea kupambana na magendo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha wanalinda viwanda vya ndani na afya za walaji.

Amesema ili kufanikisha hilo ataunda timu ya wataalamu kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanda vya mafuta na waingizaji ili kutafuta suluhisho la pamoja na la kudumu kupambana na magendo.

“Kila bidhaa inayoingizwa nchini lazima tushirikiane na vyombo vingine kusimamia ubora, lakini mafuta yanayoingia kinyume cha utaratibu ni hatari pia kwa afya za walaji, wanaweza kupata athari mbalimbali maana hiki ni chakula” amesema.

Amefafanua mbali na   kuundwa kwa timu hiyo wataendelea  kufanya doria endelevu ili kuhakikisha hakuna magendo yanayoingia nchini kupitia forodha.

Amesema TRA haizuii uingizwaji wa mafuta nchini kwani  yanayozalishwa hayakidhi mahitaji ya nchi lakini kinachotakiwa ni kufuata utaratibu wa kuingiza mafuta hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *