
Arusha/Dar. Jitihada za Kampuni ya Unilever Tea Tanzania Limited kujinusuru katika malipo ya kodi ya zaidi ya Sh27 bilioni zimegonga ukuta baada ya Mahakama ya Rufani kupiga muhuri wa mwisho wa amri ya kulipa kodi hiyo.
Mahakama hiyo imeitupilia mbali rufaa iliyoikata kampuni hiyo dhidi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikipinga uamuzi wa Baraza la Rufaa la Kodi (TRAT).
Hukumu ya rufaa hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu lililoisikiliza, likiongozwa na Jaji Gerald Ndika (kiongozi wa jopo), Dk Lilian Mashaka na Paul Ngwembe, baada ya kujiridhisha kuwa sababu za rufaa alizoziwasilisha mrufani (Unilever) hazikuwa na mashiko kisheria.
Kwa uamuzi huo wa mahakama hiyo ya juu kabisa, uliotolewa Desemba 12, 2025, ambao nakala yake imewekwa katika tovuti ya Mahakama, ni muhuri wa mwisho wa amri dhidi ya kampuni hiyo kulipa kodi hiyo.
Awali, kampuni hiyo ilikata rufaa katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) dhidi ya Kamishna wa TRA, ikipinga makadirio iliyopewa ya kodi ya jumla ya Sh27 bilioni.
Makadirio hayo yalitokana na ukaguzi uliofanywa na TRA, ambayo ilibaini kulikuwa na mapato ya bidhaa zilizouzwa nje ya nchi ambayo hayakuripotiwa, na mapato yaliyoripotiwa kuwa chini ya kiwango halisi.
Baada ya kupewa makadirio hayo ya kodi, kampuni hiyo iliwasilisha maelezo kwa kamishna kuwa tofauti zilizobainishwa zilitokana na matumizi ya ankara za muda wakati wa kusafirisha chai kwenda kwenye mnada wa Mombasa, nchini Kenya, ambako bei halisi hujulikana baada ya mauzo kufanyika.
Hata hivyo, kamishna hakukubaliana na utetezi huo, hivyo kampuni hiyo ikakata rufaa TRAB kupinga makadirio hayo.
TRAB, katika uamuzi wake, ilitupilia mbali rufaa hiyo badala yake ikakubaliana na makadirio hayo ya kamishna, lakini kampuni hiyo haikuridhika na uamuzi huo.
Hivyo, kampuni hiyo ikakata rufaa TRAT kupinga uamuzi huo wa TRAB, ambako pia ilikwaa kisiki, ndipo ikakata rufaa hiyo Mahakama ya Rufani ikipinga uamuzi huo wa TRAT.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Wakili wa mrufani, Stephen Axwesso, alikuwa na dhima ya kuthibitisha kuwa tathmini ya TRA ilikuwa na makosa.
Alidai kuwa kampuni hiyo ilitekeleza wajibu huo na kwamba mabaraza hayo hayakuzingatia ushahidi uliowasilishwa, na kuiomba mahakama hiyo ifanye tathmini upya ya ushahidi.
Mawakili wa mjibu rufaa, Wakili wa Serikali Mkuu, Carlos Mbingamno na Wakili wa Serikali, Colman Makoi, walipinga rufaa hiyo na kueleza kuwa mrufani aliitaka mahakama kuchunguza upya ushahidi uliorekodiwa, na kuwa hiyo si hoja ya kisheria.
Walidai kuwa mrufani alishindwa kutoa ankara za mwisho ambazo zingeonesha bei halisi zilizopatikana kwenye mnada.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake imeunga mkono uamuzi wa TRAT na TRAB na kukubaliana na msimamo wa TRA kuwa kampuni hiyo ilishindwa kuwasilisha ushahidi wa nyaraka, hususan ankara za mwisho, na kuthibitisha madai yake.
Jaji Ndika, aliyeandika hukumu hiyo kwa niaba ya jopo hilo, amesema hakukuwa na hoja za kisheria bali ilitaka Mahakama ichunguze upya masuala ya ukweli na tathmini ya ushahidi, jambo ambalo haliruhusiwi kisheria katika rufaa za aina hiyo.
“Kwa kuzingatia yote yaliyoelezwa hapo juu, tunaungana na wakili Mbingamno kwamba rufaa ya sasa, inayopinga tathmini ya baraza juu ya ushahidi na hitimisho lake kwamba mrufani hakutimiza mzigo wake wa uthibitisho, haiwasilishi hoja mahsusi ya kisheria,” amesema Jaji Ndika.
Amesema kuwa hoja ya wakili Axwesso kwamba baraza lilielewa vibaya ushahidi uliowasilishwa na hivyo kufikia hitimisho potofu haina mashiko.
Pia amesema kuwa wakili Axwesso hakubainisha ni kwa namna gani ushahidi ulitathminiwa vibaya wala ni kwa njia gani hitimisho lililopingwa lilikuwa lisilo la busara au lisilo na mantiki.
“Ni muhimu kusisitiza kuwa rufaa kutoka baraza zinapaswa kujikita tu katika masuala ya kisheria. Kwa maneno mengine, maswali yanayohusu tathmini ya ushahidi ni ya ukweli kimsingi na huishia katika baraza, kwa kuwa kimsingi si masuala ya kisheria,” amesema Jaji Ndika na kuongeza;
“Tunafikia hitimisho kwamba rufaa hii haina mashiko, na hivyo tunaifutilia mbali kwa gharama.”