Dar es Salaam. Hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pamoja na ongezeko kubwa la mapato yatokanayo na mauzo ya nje, zimechangia kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania na kuifanya iwe thabiti dhidi ya misukosuko ya soko la fedha za kigeni iliyoshika kasi katikati ya mwaka huu.

Licha ya shinikizo endelevu la uchumi wa dunia na kuongezeka kwa mahitaji ya dola za Marekani kulikofanya shilingi kudhoofika hadi kufikia viwango vya chini Mei mwaka huu, BoT imefanikiwa kuielekeza fedha hiyo kwenye mkondo wa utulivu kuelekea mwishoni mwa mwaka huu.

Takwimu rasmi zinaonesha shilingi iliyokuwa ikibadilishwa kwa wastani wa Sh2,454.04 kwa Dola 1 ya Marekani Januari 2025, kabla ya kudhoofika na kufikia Sh2,697.17 Mei, ilipata nafuu na kufikia kiwango cha Sh2,440.75 hadi kufikia Ijumaa iliyopita.

Kuimarika huku kunachangiwa na uamuzi wa BoT kuingiza Dola 175 milioni za Marekani katika soko la ubadilishaji fedha za kigeni kati ya benki (Interbank Foreign Exchange Market – IFEM) Mei hadi Desemba 2025 kupitia minada ya fedha za kigeni.

Katika kipindi hicho, BoT imeingiza sokoni Dola 140milioni za Marekani, huku benki za biashara zikiwasilisha maombi ya ununuzi yenye jumla ya Dola 264.5milioni. Kati ya kiasi hicho, BoT imepokea na kuuza Dola 175 milioni.

Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro akizungumzia hilo, amesema uingiliaji huo ulilenga kufikia malengo mbalimbali ya kisera, ikiwamo kupunguza misukosuko ya muda mfupi ya viwango vya ubadilishaji fedha, kuongeza akiba ya fedha za kigeni, kusaidia utekelezaji wa sera ya fedha na kuongeza ukwasi katika mfumo wa kifedha.

Amesema hatua hizo zimefanyika chini ya mfumo wa IFEM kwa kuzingatia Sera ya Uingiliaji wa Soko la Fedha za Kigeni ya mwaka 2023.

“Shilingi ilikumbwa na shinikizo kubwa zaidi Mei, wakati benki ziliwasilisha maombi ya dola yaliyokuwa zaidi ya mara mbili na nusu ya kiasi kilichokuwa kinapatikana sokoni,” amesema Akaro.

Hata hivyo, amesema kuanzia Juni 2025 shinikizo lilianza kupungua baada ya BoT kuongeza kwa kiasi kikubwa dola sokoni.

“Kufikia robo ya nne ya mwaka, uingiliaji uliofanyika Oktoba na Novemba uliifanya shilingi kubadilishwa ndani ya wigo mwembamba zaidi, ishara ya kudhibitiwa kwa kasi kwa mporomoko uliokuwa unasukumwa na matarajio ya kubahatisha,” amesema.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Akaro amesema hatua hizo zimeimarisha uthabiti wa viwango vya ubadilishaji, kuongeza shughuli za soko na kuimarisha imani ya wadau. Ametoa mfano kuwa wastani wa mauzo ya kila siku katika soko la fedha za kigeni ulifikia Dola 65 milioni, Mei 2025, huku shilingi ikionesha mwelekeo wa kuimarika.

Mbali na hatua za moja kwa moja za benki kuu, Akaro amesema shilingi ilinufaika pia na mwenendo mzuri wa mauzo ya nje.

Mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa asilimia 38.9 na kufikia Dola 4.59 bilioni ilipofika Oktoba, 2025 yakichochewa na bei za juu za kihistoria katika soko la dunia.

“Kwa jumla, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yalifikia Dola 17.05 bilioni katika mwaka ulioishia Oktoba 2025, ikilinganishwa na Dola 15.13 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2024,” amesema.

Amesema mazao kama tumbaku na korosho nayo yaliongezeka kwa asilimia 25.2 na kuingiza Dola 1.43 bilioni, huku mauzo ya nafaka kwenda nchi jirani yakifikia Dola 312.5milioni.

Mchambuzi wa masuala ya fedha, Christopher Makombe, amesema uimara wa shilingi mwaka 2025 umetokana na mchanganyiko wa sababu za kimuundo na nguvu za soko.

Amesema mapato thabiti ya dhahabu, ambayo bei yake ilifikia kilele cha Dola 4,380 kwa aunzi moja ya troy, pamoja na usimamizi makini wa ukwasi, vilisaidia kupunguza shinikizo la kubahatisha.

Amesema hali hiyo imesaidia kuepusha mabadiliko makubwa ya uwiano wa Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania.

Ameongeza kuwa kwa kiwango cha sasa cha akiba ya fedha za kigeni kinachoshikiliwa na BoT na matarajio ya kuendelea kupanda kwa bei ya dhahabu, uthabiti wa shilingi kwa mwaka 2026 unaonekana utakuwa wa uhakika zaidi.

Juhudi za kuimarisha shilingi zimeimarishwa pia na msimamo thabiti wa BoT kuhusu sera ya kupunguza matumizi ya dola katika uchumi wa ndani.

Mchambuzi wa sekta ya fedha, Kelvin Mkwawa amesema agizo la mdhibiti linalotaka miamala yote ya ndani kufanyika kwa shilingi, limepunguza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya Dola za Marekani.

Mkwawa amesema kudhibiti mikopo ya dola na kuwataka wafanyabiashara wa ndani kukopa kwa shilingi, pia kumeondoa mahitaji bandia ya dola ambayo mara nyingi huchochea kuyumba kwa viwango vya ubadilishaji fedha.

Katika mahojiano na The Citizen yaliyofanyika Oktoba, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alisema benki kuu itaendelea kufuatilia kwa karibu nafasi za mizania za benki zote za biashara ili kuhakikisha soko la fedha za kigeni linafanya kazi kwa utulivu na ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *