UNAWEZA kusema winga Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ gari limewaka akiwa kwao DR Congo kufuatia kasi yake aliyonayo ya upachikaji mabao.

Winga huyo Mkongomani aliyewahi kuitumikia Yanga kwa kipindi kifupi alipotua katika dirisha dogo la msimu uliopita akitokea AS Vita na kuondoka mwishoni wa msimu wa 2024-2025 kwa sasa yupo FC Les Aigles du Congo inayoshiriki Ligi Kuu ya DR Congo (Linafoot Ligue 1) aliyojiunga nayo Septemba Mosi mwaka huu.

Katika ligi hiyo, wakati chama la Ikangalombo likishika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya vinara AS Vita Club kwa tofauti ya pointi nne, winga huyo amehusika katika mabao 21 akicheza mechi kumi ambapo amefunga 15 na asisti sita.

Kasi hiyo ya ufungaji pengine inaweza kuwashtua wengi kwani Ikangalombo wakati yupo Yanga akikaa kwa kipindi cha miezi sita, alicheza mechi sita za ligi, hakufunga bao zaidi ya kutoa asisti mbili.

Katika mechi hizo sita za ligi akiwa Yanga alitumika kwa dakika 136 ambapo alikuwa sehemu ya timu hiyo iliyoshinda Kombe la Muungano, Kombe la FA na Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025.

IK 01

Ikangalombo hakuwahi kuanza kikosi cha kwanza wala kucheza zaidi ya dakika 30 angalau mechi moja ya ligi wakati yupo Yanga hali iliyoonyesha hakuwa mchezaji muhimu sana kwani alianza kuonekana dhidi ya Pamba Jiji akitokea benchini akichukua nafasi ya Clement Mzize wakati Yanga ikishinda mabao 3-0, Februari 28, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo alitumika kwa dakika 21.

Mechi iliyofuata ilikuwa ni Aprili 7, 2025 ambapo Yanga iliichapa Coastal Union, Ikangalombo alitumika kwa dakika 30, kisha Aprili 10, 2025 akaingia dakika 23 za mwisho Yanga ikiichapa Azam mabao 2-1.

IK 02

Dhidi ya Fountain Gate ambaoo Yanga ilishinda 4-0, Aprili 21, 2025, alicheza kwa dakika 25 akitokea tena benchini na kutoa asisti moja kwa Clement Mzize, kisha mechi mbili zilizofuatia ambazo Yanga ilipata ushindi wa kufanana wa mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons (Juni 18, 2025) alicheza kwa dakika 17 na Dodoma Jiji (Juni 22, 2025), alitumia dakika 20, akitoa asisti ya bao la mwisho kwa Maxi Nzengeli.

“Nguvu ya akili na udhibiti hutufundisha kila kitu maishani. Ikiwa akili yako inadhibiti mambo, unaweza kufanya chochote unachotaka. Hakuna kinachoweza kubadilika ikiwa hutaki kubadilika. Kila kitu kinaweza kubadilika ukitaka, kwa hiyo yote ni nguvu ya akili,” amenukuliwa akisema Ikangalombo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *