WAKATI mwenyewe akiwa njiani kuja Tanzania ili kuanza kuinoa Simba, inadaiwa kuwa ujio wa kocha mkuu mpya, Steve Barker umezuia panga lililokuwa lipite kwa mastaa wa timu hiyo hadi kwanza awaone wachezaji wote kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza Desemba 28.

Simba ilimtambulisha rasmi kocha huyo wa zamani wa Stellenbosch ya Afrika Kusini kuja kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dimitar Pantev aliyetemwa hivi karibuni ambaye kabla ya kuondoka alitoa mapendekezo ya kupitishwa kwa panga kwa baadhi ya mastaa kupitia dirisha dogo la usajili.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa mpango huo kwa sasa umesitishwa kwa muda, akisubiriwa kocha Barker ili kuitumia michuano ya Mapinduzi 2026 kama sehemu ya tathmini yake kabla ya kubariki panga hilo.

Awali, kulikuwa na majina ya wachezaji wa timu hiyo yaliyowekwa mezani yakijadiliwa ili kuachana nayo katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa mapema Januari mwakani ili kutoa nafasi kwa wachezaji wapya kwa mujibu wa ripoti ya aliyekuwa meneja wa timu hiyo, Pantev.

Hata hivyo, ujio wa Barker umebadili mwelekeo wa mambo ndani ya klabu hiyo na taarifa kutoka kwa mmoja wa vigogo wa klabu hiyo ni kwamba majina manne yaliyokuwa yakijadiliwa ili kufyekwa, yatasubiri uamuzi wa kocha huyo raia wa Afrika Kusini.

Taarifa hizo za ndani zinasema majina hayo manne yaliyoandaliwa kwa kila mmoja alikuwa na sababu ya kupendekezwa kuachwa, lakini kocha mpya ameomba kuwafanyia tathmini upya mastaa hao.

“Kila kitu kimesimama kwanza, tunasubiri timu irudi kambini na kushiriki Kombe la Mapinduzi hapo atapata muda wa kuwafahamu wachezaji waliopo ambao hawajaenda Morocco kucheza fainali za AFCON, kisha kuona nini cha kufanya katika dirisha hilo,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.

Miongoni mwa majina yaliyopendekezwa kufyekwa kikosini ni kiungo mshambuliaji Neo Maema, aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miezi sita uliokuwa na kipengele cha kuongezewa endapo angeonyesha kiwango cha juu.

Mbali na Maema, jina jingine lililokuwa mezani ni la beki Chamou Karaboue, lakini Barker bado hajatoa uamuzi wa mwisho.

Pia linatajwa jina la winga Joshua Mutale, ambaye licha ya kupewa nafasi mara kadhaa, amekuwa akishindwa kuonyesha uwezo wa kuibeba timu, sambamba na straika Steven Mukwala, aliyemaliza msimu uliopita akiwa na mabao 13 na asisti tatu, lakini msimu huu amekuwa chini ya kiwango.

Simba ilikuwa tayari inaanza mchakato wa kusaka mshambuliaji mwingine, huku Mukwala akitajwa kupewa mkono wa kwaheri endapo mbadala atapatikana na pale dili la kuuzwa lililokuwa likielezwa tangu mwanzoni mwa msimu.

Kuhusu mwelekeo wa usajili, aliyekuwa Meneja Mkuu wa Simba, Pantev alinukuliwa na Mwanaspoti akisema; “Simba ina malengo makubwa, hivyo ni lazima isajili wachezaji watakaoendana na hadhi ya klabu kwa maana ya viwango vya juu.”

Kwa mujibu wa ratiba ya Mapinduzi, Simba imepangwa Kundi B na itatupa karata ya kwanza dhidi ya dhidi ya Muembe Makumbi City kabla ya kucheza na Fufuni siku mbili baadaye katika michuano hiyo inayoshirikisha timu 10 zikiwamo Yanga, Singida BS, Azam na TRA United kutoka Tanzania Bara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *