Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa ameitaja hatua ya Misri ya kuidhinisha makubaliano ya ununuzi wa gesi kutoka kwa utawala wa Israel kuwa ni uungaji mkono wa nchi hiyo kwa mauaji ya halaiki yanayofanywa na Wazayuni huko Gaza.

Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa, huku akikosoa vikali makubaliano ya gesi kati ya Misri na utawala wa Israel, amesema kwamba makubaliano hayo yanaonyesha uungaji mkono wa Cairo kwa Tel Aviv katika mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Albanese ameongeza: “Misri inaweza kusema chochote inachotaka, lakini kununua gesi yenye thamani ya dola bilioni 35 kutoka kwa utawala wa Israel ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.”

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kwamba, makubaliano hayo ni ishara ya wazi ya uungaji mkono kwa utawala wa Israel katika mauaji ya halaiki ya Wapalestina.

Kadhalika Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi hiyo ya Kiarabu kutoweka kipaumbele maslahi ya kiuchumi kuliko maadili ya kibinadamu.  

Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu kutangaza kuwa, serikali yake imeidhinisha makubaliano makubwa ya uuzaji wa gesi asilia kwa Misri yenye thamani ya karibu dola bilioni 35, akielezea kwamba makubaliano hayo ni makubwa zaidi katika historia ya Israel kwa upande wa thamani na ujazo wa usafirishaji nje.

Misri mpaka sasa inasita kutoa maelezo ya kina kuhusu makubaliano hayo, ingawaje baadhi ya maafisa wake wanasisitiza kuwa, mkataba huo wa kibiashara na Tel Aviv haumaanishi kuwa Cairo imeacha kutetea kadhia ya Palestina.

Maoni ya umma ya Misri yanafungamana kihistoria na suala la Palestina, na kuanza vita vya Gaza baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023 ulikuwa mwanzo wa mabadiliko katika sera za ndani na za kigeni za Misri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *