
Viongozi wa nchi kadhaa Afrika siku ya Jumapili walitaka juhudi za kikanda zipewe kipaumbele katika kutatua mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku mipango ya kimataifa ikipewa nafasi ya usaidizi.
Wito huo ulitolewa katika mkutano wa kilele wa kikanda wa siku moja uliofanyika huko Entebbe nchini Uganda, ambao uliwaleta pamoja viongozi na wajumbe ili kushughulikia hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya mashariki mwa DRC na kuenea katika eneo la Maziwa Makuu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda John Mulimba alisema washiriki walikubaliana kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinapaswa kuongoza juhudi za amani ili kushughulikia mgogoro unaoongezeka.
Kw upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Vincent Biruta alisema changamoto kuu ipo katika ukosefu wa utekelezaji wa makubaliano ambayo tayari yamefikiwa. Alielezea makubaliano ya Washington na mipango ya amani ya Doha kama mifumo inayofaa zaidi ya kushughulikia pande zote mbili za ndani na za kikanda za mgogoro huo.
Mapema mwezi huu, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zilisaini makubaliano ya yaliyosimamiwa na Marekani mjini Washington, yakilenga kukomesha miongo ya mapigano. Hata hivyo, mapigano yamezidi kushika kasi Mashariki mwa DRC, huku waasi wa kundi la March 23 Movement (M23) wakisonga mbele na kutwaa ngome mpya.
Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump, yamekosolewa vikali na wachambuzi wengi wanaosema yamelenga zaidi kurahisisha uporaji na uhamishaji wa madini adimu kutoka mashariki mwa DRC kuliko kuleta amani ya kweli katika eneo hilo. Trump mwenyewe alisema baada ya mapatano hayo, makampuni ya kiteknolojia ya Marekani yataweza kuchimba madini ya DRC, jambo linaloweka wazi nia yake ya kupora madini ya nchi hiyo.