
Serikali ya Nigeria imetangaza kufanikiwa kuwaokoa wanafunzi 130 wa shule waliotekwa na watu wenye silaha kutoka shule ya Kikatoliki mwezi Novemba.
Msemaji wa Rais wa Nigeria, Sunday Dare, alitoa taarifa kupitia chapisho kwenye X akisema: “Wanafunzi 130 waliotekwa katika jimbo la Niger wamepatikana, hakuna aliyebakia.”
Mwishoni mwa Novemba, mamia ya wanafunzi na wafanyakazi walitekwa katika shule ya bweni ya pamoja ya St. Mary’s, iliyoko kaskazini mwa jimbo la Niger.
Chanzo cha Umoja wa Mataifa kililiambia AFP kwamba “kundi lililobaki la wasichana au wanafunzi wa shule ya sekondari litapelekwa Minna,” mji mkuu wa jimbo la Niger, siku ya Jumanne.
Idadi halisi ya waliotekwa na waliobaki kushikiliwa haijawa wazi tangu shambulio hilo lililotokea katika kijiji cha Papiri.
Nigeria imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za usalama, ikiwemo utekaji nyara wa wanafunzi, mashambulizi ya kigaidi na mapigano baina ya wafugaji na wakulima.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, hivi karibuni alitangaza hali ya dharura ya usalama nchini kote.
Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu na kuchapishwa kupitia mtandao wa kijamii X (zamani Twitter) tarehe 26 Novemba, Rais Tinubu aliagiza idara ya polisi kuajiri askari wapya 20,000 ili kukabiliana na ukosefu wa usalama, na kufanya idadi ya askari wanaopangwa kuajiriwa mwaka huu kufikia 50,000.
Mapema Novemba, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Nigeria kwa madai ya mauaji ya Wakristo. Serikali ya Nigeria imepinga madai hayo, ikisema hayana uhalisia kwani Wanigeria wote, wawe Wakristo au Waislamu, ni wahanga wa ukosefu wa usalama.