Taarifa hiyo imetolewa siku ya Jumapili na waziri wa fedha wa Israel mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Bezalel Smotrich aliyetaja kuwa kwa sasa makazi hayo yamefikia idadi ya 69. Smotrich ambaye amekuwa mstari wa mbele kuitetea ajenda ya upanuzi wa makazi hayo ya walowezi, amesema hiyo ni rekodi mpya katika miaka ya hivi karibuni.

Hatua hiyo inaongeza idadi ya  makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi  kwa karibu asilimia 50 katika uongozi wa serikali ya sasa yenye siasa kali za mrengo wa kulia. Mwaka 2022, kulikuwa na makazi 141 katika Ukingo wa Magharibi na sasa idadi hiyo imefikia 210, hii ikiwa ni kulingana na kundi la “Peace Now”, linalohimiza amani, kufuatilia na kupinga uwepo wa makazi hayo yanayozingatiwa kuwa kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar ametoa wito kwa Wayahudi waliopo katika nchi za Magharibi kuhamia Israel ili kuepuka vitendo vinavyoongezeka vya  chuki dhidi ya Wayahudi, ikiwa ni wiki moja baada ya watu 15 kupigwa risasi na kuuawa wakati wa sherehe ya Kiyahudi ya Hannukah katika ufukwe wa Bondi mjini Sydney, Australia.

Shinikizo la kuendelea kutekeleza mpango wa usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza

Seneta wa Marekani Lindsey Graham akizungumza karibu na rais Trump
Seneta wa Marekani Lindsey Graham ( kulia) alifanya ziara huko Israel siku ya Jumapili, na hapo alikuwa akizungumza karibu na rais Donald TrumpPicha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Yote hayo yanaripotiwa wakati Marekani imekuwa ikizishinikiza Israel na Hamas kuendelea na awamu ya pili ya mpango wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa  Gaza , ambao ulianza kutekelezwa Oktoba 10, 2025. Mpango huo unaosimamiwa na Marekani unasisitiza “uwezekano” wa kutafuta namna ya kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina, jambo linalokinzana na utanuzi wa makazi hayo ya walowezi.

Katika hatua nyingine, Seneta wa Marekani Lindsey Graham alifanya ziara huko Israel siku ya Jumapili na ameyawashutumu makundi ya Hamas na Hezbollah ya Lebanon kwa kujiimarisha upya huku akisisitiza kuwa kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina lilikuwa likiimarisha mamlaka yake huko Gaza na kutoa wito wa hatua kadhaa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa haraka wa kuipa Hamas muda wa kufikia lengo la kuweka chini silaha.

” Tofauti na hivyo, nitamuunga mkono Rais Trump kuiruhusu Israel kuendelea na operesheni yake ya kuitokomeza Hamas, ” alisema Seneta huyo wa Marekani.

Licha ya makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano kutekelezwa huko Gaza kwa zaidi ya miezi miwili sasa, hali ya maisha bado ni mbaya mno katika ukanda huo ulioharibiwa vibaya na vita.

(Vyanzo: Mashirika)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *