Wachunguzi wa Russia wamethibitisha kuwa Mkuu wa Kurugenzi ya Uendeshaji ya Mafunzo ya Vikosi vya Ulinzi vya Russia ameuawa baada ya mada ya mlipuko ilioyokuwa imetegwa chini ya gari yake kulipuka katika wilaya ya Yasenevo kusini mwa mji mkuu wa Russia, Moscow.

Luteni Jenerali Fanil Sarvarov, aliyekuwa na umri wa miaka 56, ameuawa mapema leo Jumatatu akiwa njiani kuelekea kazini.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa mada ya mlipuko ilitegwa chini ya gari ya afisa huyo wa jeshi la Russia aina ya Kia Sorento na ililipuka baada ya gari kuanza kuondoka.  

Msemaji rasmi wa Kamati ya Uchunguzi ya Russia, Svetlana Petronko amesema kuwa mamlaka husika zinafuatilia mauaji hayo. Kamati hiyo imesema, kuna uwezekano Idara ya Ujasusi ya Ukraine imehusika katika mauaji hayo. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Luteni Jenerali Igor Kirillov Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nyuklia, Baolojia na Kemikali vya Jeshi la Russia aliuawa na kifaa cha mlipuko kwenye skuta ya umeme nje ya makazi yake, siku moja baada ya Kiev kuwasilisha mashtaka ya jinai dhidi yake.

Aidha mwezi Aprili mwaka juzi, Maxim Fomin, mwanablogu wa kijeshi wa Russia aliuawa wakati sanamu lilipolipuka kwenye mkahawa huko St. Petersburg. 

Luteni Jenerali wa jeshi la Russia ameuawa leo katika hujuma ya mlipuko huku vita vikiendelea huko Ukraine na katikati ya mazungumzo ya maafisa wa Russia na wenzao wa Marekani huko Miami kwa lengo la kuchunguza njia za kuhitimisha vita kati ya Russia na Ukraine.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *