KIUNGO wa Yanga, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amesema mabonanza yanayofanywa na wachezaji kipindi cha mapumziko ya Ligi Kuu Bara ni chachu ya kuboresha ushindani na kuwakutanisha pamoja.

Sure Boy alifunguka hayo muda mchache baada ya mechi ya hisani ya Magomeni Foundation ililofanyika kwenye Uwanja wa Mzimuni Magomeni, iliyowakutanisha wachezaji wanaocheza Ligi Kuu na Magomeni Combain.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sure Boy amesema tofauti na kwenye ligi, wakikutana wao ni marafiki na wanakumbushana nini wafanye ili wawe bora kitu ambacho kinawajenga.

“Ukiondoa ligi ambayo tukicheza tunakuwa wapinzani mtaani ni marafiki na tumekuwa tukipeana michongo ya kufanya hata mambo mazuri ya kukuza na kuboresha uwezo uwanjani. Huwa tunashirikishana. Nikiharibu uwanjani leo Himid Mao, Hassan Dillunga ananipigia wananiambia pale ulizingua, hivyo hivyo nikifanya vizuri.”

“Pia kuna maisha baada ya mpira, tunatakiwa kuishi vizuri ili tujenge kesho njema. Nashukuru wadau wameitika na kutupa sapoti kwa kujitokeza kwa wingi kutupa sapoti.”

Akizungumzia mechi hizo ambazo zimekuwa zikifanyika kwa miaka ya hivi karibuni zikihusisha wachezaji wakiwa mapumzikoni amesema ni mazuri kwao kuwakutanisha pamoja kupeana mbinu tofauti na kazi yao hiyo wakiwa kwenye ajira zao kwenye timu za ligi.

“Tukikutana na kucheza timu pamoja kwa mchanganyoko kutoka wachezaji kutoka timu tofauti inatujenga kuwa tunatakiwa kupendana na kuheshimiana nje ya mpira sisi ni ndugu nimecheza na Mao tukiwa pamoja Azam FC nimekutana naye hapa ni baada ya muda mrefu lakini kuna wachezaji wameingia kwenye soka kwa kututazama sasa tunaungana nao kucheza pamoja inawajenga.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *