TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kufanya upimaji wa siku mbili wa magonjwa ya moyo bure kwa waandishi wa habari na wahariri wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kundi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amesema upimaji huo maalum utafanyika Desemba 23 hadi 24 katika tawi la JKCI lililopo Oysterbay, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyotoa kwa waandishi wa habari. Amesema huduma zitatolewa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. SOMA: JKCI yazindua mifumo ya kisasa ya miadi
Dk. Kisenge amesema vipimo vitakavyotolewa ni pamoja na ECHO, ECG, upimaji wa mafuta kwenye damu, sukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza, na kwamba huduma zote zitatolewa bure. Ameongeza kuwa pia kutatolewa elimu ya lishe na mtindo bora wa maisha, ambapo maafisa lishe watawashauri waandishi wa habari aina ya chakula, kiasi kinachofaa na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Amesisitiza kuwa kuwahudumia waandishi wa habari ni muhimu kwa sababu elimu watakayopata itaifikisha jamii kupitia kalamu zao, hivyo kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi na kupunguza gharama za matibabu kwa Serikali. Dk. Kisenge amewahimiza waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi ili kufahamu hali zao za kiafya.
