KUTOKANA na mikoa ya Kaskazini kuongoza kwa matatizo ya magonjwa ya moyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeamua kuendelea kufanya kambi maalum ya upimaji na matibabu mkoani Arusha na mikoa ya jirani. Takwimu za JKCI zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia tano ya wagonjwa 23,000 waliopata huduma wanatoka katika mikoa ya Kaskazini.
Sababu kuu zinazochangia ongezeko la maradhi ya moyo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ni pamoja na unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara, kutofanya mazoezi na matumizi ya mafuta ya wanyama. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kusogeza huduma na kutoa elimu ya afya ya moyo ili kuzuia madhara zaidi.
Dk. Kisenge amesema kambi hiyo maalum itaanza Desemba 29, 2025 hadi Januari 5, 2026, katika Hospitali ya Arusha Lutheran Central (Seliani), ambapo huduma zitatolewa kwa watoto na watu wazima kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. Ameongeza kuwa hospitali hiyo imeingia ushirikiano wa miaka 20 na JKCI, utakaowezesha huduma za moyo kupatikana karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini. SOMA: JKCI yaanza tiba kupunguza msisimko shinikizo la damu
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Moyo wa JKCI, Dk. Tatizo Wanne, amesema takribani asilimia 25 ya wagonjwa wanaohudumiwa na JKCI wanatoka Kanda ya Kaskazini, hivyo uwepo wa huduma hizo Arusha utapunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu. Naye Meneja Mawasiliano wa Bohari ya Dawa (MSD), Etty Kusiluka, amesema MSD itahakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati ili kufanikisha matibabu yote yatakayotolewa.
