Kila Mtanzania mzalendo ni muumini wa maridhianoKila Mtanzania mzalendo ni muumini wa maridhiano

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira ya dhati ya maridhiano ya kweli tangu alipoingia madarakani. Alifungua mazungumzo ya kisiasa baina ya serikali na vyama vya siasa. Hata baada ya uvunjifu wa amani Oktoba 29, 2025, serikali chini ya Rais Samia imeendelea kuamini katika maridhiano ambayo ndiyo msingi wa amani.

Akizungumza katika ibada ya kubariki wachungaji ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amebainisha msimamo wa serikali kuhusu maridhiano. Amebainisha kwamba maridhiano ya kweli si shughuli ya siku moja bali ni mchakato unaohitaji uvumilivu, ustahimilivu, unyenyekevu na ushirikiano wa wadau wote akitaja serikali, taasisi za dini, taasisi za kiraia na wananchi wote kwa ujumla.

Tunaungana na Simbachawene tukihimiza kila mdau mzalendo na mpenda maendeleo ya Tanzania, kubeba ujumbe huu kwa uzito, akitambua kwamba maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana kwa misukumo ya muda mfupi wala kwa kauli kali zinazochochea mgawanyiko.

Maridhiano ni safari ndefu inayohitaji moyo wa subira, utayari wa kusikiliza hoja za wengine, kukubali makosa pale yanapotokea na kuweka mbele maslahi mapana ya taifa badala ya maslahi binafsi au ya kikundi. Hapa ndipo busara ya serikali ya kusisitiza mazungumzo na maridhiano inapopata uhalali wake ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya mazungumzo, kushirikisha wadau mbalimbali na kusisitiza siasa za ustaarabu.

Ni ukweli ulio wazi kwamba maridhiano hayawezi kupatikana katika mazingira ya migongano, chuki na misuguano isiyoisha. Isitoshe, maridhiano si suala linalopaswa kuachiwa serikali pekee. Taasisi za dini pia zina wajibu mkubwa wa kuhubiri amani, upendo na kusameheana huku taasisi za kiraia zikitakiwa pia kutoa sauti za busara, zikihimiza mazungumzo badala ya misimamo mikali.

Wananchi nao ni sehemu ya maridhiano, wanapaswa kutambua kuwa tofauti za mawazo ni sehemu ya maisha ya kidemokrasia lakini hazipaswi kuwa chanzo cha kuvuruga amani ya nchi. Kwa mantiki hiyo, kila Mtanzania mzalendo na mpenda maendeleo ana wajibu wa kuungana na msimamo wa serikali wa kutaka maridhiano kwa maslahi mapana ya taifa.

Kuunga mkono maridhiano si udhaifu, bali ni ishara ya uzalendo wa kweli na uelewa kuwa amani ndiyo mtaji mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. SOMA: Tume ya Uchunguzi ina ‘kibarua kizito’ lakini muhimu

Ni wakati sasa kwa Watanzania wote, bila kujali tofauti zetu za kisiasa, kijamii au kiitikadi kujiuliza Tanzania kuhusu tunayoitaka. Je, tunataka taifa lenye migogoro ya kudumu au lenye mshikamano, amani na maendeleo endelevu? Jibu lake lipo wazi; maridhiano ya kweli ndiyo njia sahihi ya kulinda na kuijenga Tanzania ya leo na ya vizazi vijavyo, kila Mtanzania mzalendo ni muumini wa maridhiano ya kuliponya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *