Dar es Salaam. Wanafunzi watatu kutoka shule tofauti jijini Dar es Salaam wameshinda ufadhili wa masomo kutoka Benki ya CRDB katika msimu wa pili wa Tamasha la Watoto lililoandaliwa na Kids’ Holiday Festival, lililofanyika jijini hapa.

Katika msimu huu, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Kids’ Holiday Festival imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa watoto pamoja na wazazi au walezi wao, ikiwa ni jitihada za kuwajengea misingi ya usimamizi bora wa masuala ya kiuchumi tangu wakiwa wadogo.

Elimu hiyo hutolewa katika matamasha yote mawili yanayoandaliwa na Kids’ Holiday Festival.

Akizungumza katika tamasha la kwanza lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, amesema elimu ya fedha ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla,  hivyo inapaswa kuanza kutolewa mapema.

Amesema jamii inahitaji elimu ya fedha ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazohusiana na masuala ya kifedha, na akaeleza kufurahishwa na uwepo wa majukwaa yanayowawezesha watoto kucheza na kujifunza kwa wakati mmoja, yakiwamo mafunzo kuhusu huduma za benki.

Mnzava ameongeza kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na wadau wenye majukwaa yanayowakutanisha watoto, kama ilivyo Kids’ Holiday Festival, ili kufikisha elimu ya fedha kwa watu wengi zaidi na kujenga msingi imara wa maarifa ya kifedha kwa watoto.

Katika tamasha hilo, Benki ya CRDB imetoa ufadhili wa masomo kwa watoto watatu kama sehemu ya mchango wake katika kuunga mkono sekta ya elimu na kuwahamasisha watoto kufikia ndoto zao za kielimu.

Mnzava amewapongeza watoto wote walioshinda pamoja na wazazi wao kwa kuwahamasisha kushiriki katika tamasha hilo, huku akibainisha kuwa nafasi moja ya ufadhili ilitolewa kupitia CRDB Insurance Company, na mbili zikitolewa na Benki ya CRDB.

Walioshinda ufadhili huo ni Gabriel Festo Joseph wa Shule ya Awali na Msingi Bubble Guppies na Arabella Ambonnye Mpangala wa Shule ya Msingi Mount Kibo, shule zote za jijini Dar es Salaam, pamoja na Alvin Freddy Urio wa Shule ya Sekondari Carmel ya mkoani Iringa.

Akizungumza baada ya ushindi wa mwanawe, Pendo Peonson, mama mzazi wa Alvin, amesema matamasha ya aina hiyo yana faida kubwa kwa watoto kwa kuwa huwapa fursa ya kujifunza, kucheza na kupanua wigo wa marafiki.

Amesema licha ya mwanawe kutokuwa na akaunti ya benki awali, wamefanikiwa kufungua akaunti wakati wa tamasha hilo, na kuwahimiza wazazi wengine kutumia majukwaa kama hayo kwa manufaa ya watoto wao.

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kids’ Holiday Festival, Geraldine Mashele, amesema tamasha hilo ni jukwaa muhimu kwa watoto kukuza vipaji vyao na kupata maarifa yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Amesema ushirikiano na Benki ya CRDB umesaidia kuwafikia watoto wengi zaidi na kuwajengea misingi ya kujisimamia kifedha wanapokua.

Geraldine ameongeza kuwa tamasha hilo ni sehemu ya mkakati mpana wa Kids’ Holiday Festival wa kuwawezesha watoto na kwamba, katika siku zijazo, wanapanga kuanzisha klabu za watoto mashuleni zitakazowawezesha kujifunza kupitia michezo na shughuli shirikishi.

Imeelezwa kuwa tamasha la pili la Kids’ Holiday Festival litafanyika Desemba 27, 2025, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambako ufadhili mwingine wa masomo utatolewa kwa watoto watakaoshiriki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *