
Arusha. Jalada la mashtaka kuhusu tuhuma zinazomkabili Anna Melami anayedaiwa kumjeruhi mumewe kwa kumkata uume, limepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa hatua zaidi.
Anna anatuhumiwa kumjeruhi mumewe, Baraka Melami (40), usiku wa Novemba 19,2025 walipokuwa wamelala nyumbani kwao katika Kijiji cha Olevolosi,Kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru.
Melami alidai usiku wa saa saba kasoro wakiwa wamelala na mke wake alianza kumtomasa na kumshika sehemu za siri, kuzikata na kutupa chini ya mvungu wa kitanda.
NPS ndiyo ofisi yenye jukumu la kuamua mtuhumiwa ashtakiwe na kwa kosa lipi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Desemba 22, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema jalada hilo limepelekwa ofisi za NPS kwa hatua zaidi na mwanamke huyo bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi.
“Kwa sasa taarifa nilizonazo jalada limepelekwa ofisi za NPS kwa hatua zaidi,” amesema SACP Masejo.
Tukio lilivyokuwa
Awali, Melami alilazwa na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Selian wilayani Arumeru, akisimulia tukio hilo lilivyotokea, alidai kuwa, “usiku alianza kunitomasa sehemu za siri na iliposimama akachukua kisu akaikatia chini yote, akanifunika na blanketi kubwa akaanza kuninyonga, nikapambana naye hadi nikaweza kutoka naye nje nikipiga kelele, watu wakaja kunisaidia wakanitoa na kunileta hospitalini.”
“Hatukuwa na ugomvi wowote tunafanya kazi ya kuuza dukani kwetu, tulilala vizuri hakuna aliyekuwa na shida na mwenzake. Mimi nina mtoto mmoja tu na kwa kuwa tuna kitanda kimoja hapa kingine kipo dukani, mara nyingi mke wangu alikuwa analala na mtoto kule akihitaji tendo la ndoa anakuja tunalala kwenye kitanda chetu,” alisema.
Melami alieleza kuwa mchana kabla ya tukio hilo walichimba choo nyumbani kwao, wakaendelea na biashara ya kuuza duka hadi jioni walipolifunga kisha wakaenda kulala.
“Mimi sikuwa nimevua nguo kulikuwa na baridi na nilikuwa nimechoka hivyo nililala na nguo na alivyokuja akanifunika na blanketi, akafungua zipu akashusha suruali kidogo. Baada ya tukio wakati nahangaika damu ilimwagika na hata nilipojaribu kutoka nje aliendelea kunifuata akininyonga,” alielezea.
Alidai baada ya tukio hilo mkewe alijifanya amepoteza fahamu baada ya ndugu na majirani kutoka, waliwachukua wote wawili na kuwapeleka hospitali na kuwa wakati anajaribu kumnyonga alimwambia anataka kumuua halafu na yeye anajiua kwa kunywa sumu.
“Hatujagombana karibu miezi mitatu na baada ya kufika hapa wakauliza hiyo sehemu ya siri ilipo na ndugu zangu walirudi nyumbani kuitafuta na walipoileta madaktari walisema imeshapoa haifai kurudisha tena,” alisema.
Alidai kuwa siku hiyo mkewe alifungulia redio kwa sauti kubwa tofauti na siku zingine ambapo hata alipokuwa akijaribu kupiga kelele kuomba msaada nje sauti haikuweza kusikika.