
Utafiti uliofanywa na kampuni ya NordPass umeonesha kuwa namba 123456 imeendelea kushika nafasi ya kwanza kuwa nenosiri lililotumiwa zaidi duniani mwaka 2025, licha ya tahadhari za mara kwa mara kutoka kwa wataalamu wa usalama wa mtandao kuhusu hatari ya kutumia nenosiri dhaifu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, passwords rahisi kama 12345, 12345678 na 123456789 bado zinatumika kwa wingi katika makundi yote ya umri, hali inayowaacha watumiaji katika hatari kubwa ya kudukuliwa.
Hali hiyo imeonekana pia kwa watumiaji vijana, ambao mara nyingi huchagua nenosiri rahisi kwa lengo la kulikumbuka kwa urahisi katika matumizi yao ya kila siku ya kidijitali.
Wataalamu hao wanaeleza kuwa matumizi ya nenosiri rahisi yamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la visa vya wizi wa taarifa binafsi, udukuzi wa akaunti za mitandao ya kijamii na mifumo ya kifedha, hasa katika kipindi ambacho huduma nyingi zimehamia mtandaoni.
NordPass ni huduma ya kidijitali ya kusimamia nenosiri (password manager) iliyozinduliwa mwaka 2019, ikishirikiana na huduma ya VPN, ikiwa na lengo la kuwasaidia watumiaji kupanga, kuhifadhi na kulinda passwords pamoja na kumbukumbu zao muhimu kwa njia salama.