
Soka la kisasa linahitaji mawinga ambao wana uwezo wa kuchezesha timu na kufunga mabao kadri wanavyopata nafasi.
Mwananchi limefanya mahojiano na Ismail Aidan Mhesa ambaye amefunguka mambo mbalimbali, ikiwa ni kujimwagia sifa kuwa ni winga wa kisasa anayesifika kwa mbio lakini pia ana uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira katika kuhakikisha anatengeneza nafasi na kufunga.
UFUNDI NDIO MPANGO
Mhesa anasema kuwa yeye ni winga ambaye anaweza kuipa timu matokeo mazuri na pia kufurahisha jukwaa.
“Mimi ni winga niliyekomaa. Ukitaka tukimbizane pumzi ipo, lakini pia ukitaka tucheze mpira hakuna kinachoshindikana. Mpira umezaliwa kwa ajili yangu.
“Ukiondoa kuwa na kasi ya kukimbia, napenda kuuchezea mpira, kufunga na kutengeneza nafasi na ndiyo maana najiweka kwenye kundi la mawinga waliokamilika. Yaani wanafanya kila kitu uwanjani kutokana na nafasi,” alisema Mhesa.
PACOME/NADO
Pamoja na kujimwagia sifa kwa kujiamini kuwa ana uwezo mkubwa, Mhesa hakusita kuwataja mawinga wengine bora anaovutiwa na aina yao ya uchezaji, akimtaja Pacome Zouzoua kwa nyota wa kigeni anayocheza Ligi Kuu na kwa nyota wa ndani amemtaja Idd Nado.
“Kuna mawinga wengi bora ambao wana uwezo mkubwa na ni tishio kwa timu pinzani wamepita Ligi Kuu Tanzania Bara na wanaendelea kufanya poa kwenye ligi, mfano Pacome anayekipiga Yanga ni mchezaji mzuri, anaujua mpira na kuufanya kuwa mchezo rahisi.
“Ni winga anayetumia akili sana, ana nguvu, kasi na ubora wa kucheza mpira. Kwa upande wa wachezaji wa ndani kuna Idd Kipagwile na Idd Nado, wote wamekuwa wakifanya vizuri,” alisema Mhesa.
NGASSA ALIMVUTA LIGI KUU
Mhesa amemtaja Mrisho Ngassa kuwa ndiye winga aliyemvuta kucheza soka la ushindani.
“Ni kweli mimi nimeingia kwenye soka kutokana na familia yangu kuwa katika sekta hiyo kuanzia baba yangu hadi watangulizi wangu na kaka zangu. Lakini Ngassa ndiye mchezaji aliyenifanya nipambane na kuingia kwenye mpira kutokana na namna ambavyo alikuwa anazungumzwa.
“Ukiondoa stori za mashabiki, lakini pia hata redioni alikuwa anatajwa sana. Kitu ambacho kilikuwa kinanipa nguvu ya kupambana ili na mimi niweze kuwa kama yeye. Baada ya kupata nafasi ya kucheza nilishawahi kumwambia kuwa yeye ndiye aliyenifanya nipende mpira. Ni muungwana sana, aliniambia nijitume na niamaini mazoezi nitafikia mafanikio,” anasema Mhesa.
BABA ALIMPELEKA MTIBWA
Mhesa alianza safari yake ya soka la kulipwa kupitia njia ambayo wengi huota lakini wachache huipitia. Akiwa bado kijana mwenye ndoto kubwa, alijikuta akipelekwa Mtibwa Sugar na baba yake.
“Baba ndiye aliyekuwa daraja muhimu la mimi kufika Mtibwa Sugar. Sikupelekwa na kukubaliwa kwa sababu ya historia ya baba, hapana. Nilifanya majaribio kuonwa kama nina uwezo wa kucheza hapo na nashukuru Mungu nilifanikiwa kuvuka.
“Baba alipita hapo, aliamini katika kipaji changu na ndiyo maana alinipa nafasi ya kwenda kujaribu hapo. Uzoefu wa baba ndani ya Mtibwa Sugar ulinisaidia kufungua milango, lakini haukuwa tiketi ya moja kwa moja ya kusajiliwa,” anasema.
KUIPA TAJI MTIBWA, AMEITAJA SINGIDA
Ulikuwa msimu wa 2021 ambapo Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza ilitwaa taji la FA kwa kuichapa Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, mchezo ambao Mhesa ameutaja kuwa bora kwake.
“Nimecheza mechi nyingi za ushindani na bora, lakini mechi yangu bora hadi sasa ni fainali ya FA dhidi ya Singida. Nilifunga bao muhimu na timu yangu ilipata kombe, ni mchezo ambao hautoki akilini kwangu.
“Ilikuwa mechi bora sana kwangu na nakumbuka simu zilipigwa sana baada ya huo mchezo. Kumbuka fainali ilichezwa ligi ikiwa tayari imeisha, hivyo ilitazamwa na watu wengi sana,” anasema Mhesa.
AMEMCHAMBUA KIBWANA
Pamoja na kukutana na mabeki wengi tangu aanze kucheza soka la ushindani, Mhesa amemtaja Kibwana Shomari kuwa ni beki anayehitaji akili kubwa unapokutana naye.
“Kibwana ni mzuri wa kucheza mtu na mtu. Akipewa kazi hiyo na kocha, kwa asilimia kubwa lazima aifanikishe. Nimeshawahi kukutana naye na baada ya mechi nilimfuata nikamwambia kuwa anapania sana.
“Kibwana anakaba, anaweza kupanda na kushuka naye bila kukupa nafasi. Si mzuri sana kukupa nafasi, akikuacha kidogo unaweza kumkimbia. Lakini akianza na wewe mwanzo hadi mwisho huwezi kutoa pasi sahihi au kufunga hata ukiwa ndani ya 18,” anasema Mhesa.