Tanzania kuendelea kuuza mahindi MalawiTanzania kuendelea kuuza mahindi Malawi

TANZANIA imeihakikishia Malawi kuwa ipo tayari kuendelea kushirikiana katika biashara ya mahindi. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dk Stephen Nindi amesema hayo baada ya kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Malawi, Erica Maganga jijini Lilongwe, Malawi.

Dk Nindi alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) una akiba ya zaidi ya tani 500,000 za mahindi, hivyo Tanzania ipo tayari kuendeleza uhusiano wa kibiashara na Malawi kulingana na mahitaji yao. SOMA: Bashe awatoa wasiwasi wakulima wa mahindi

Maganga ameipongeza Tanzania kwa mifumo yake ya hifadhi ya nafaka, akieleza kuwa inazingatia viwango vya ubora. Viongozi hao walijadili pia fursa za kuimarisha biashara ya mahindi na ushirikiano wa kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika hatua nyingine, ujumbe wa Tanzania ulikutana na uongozi wa NFRA wa Malawi pamoja na uongozi wa Chama cha Wauzaji na Wasindikaji wa Nafaka cha Malawi (GTPA), na kujadili fursa za kibiashara za zao la mahindi, masuala ya udhibiti wa sumukuvu na changamoto za masoko.

Wengine waliokuwa kwenye ujumbe wa Tanzania ni pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dk Andrew Komba; Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya NFRA, Robinson Meitinyiku na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Agnes Kayola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *