Uongozi wa hifadhi ya taifa ya Tarangire umetaja Sababu zinazofanya Hifadhi hiyo kuendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa mazao mapya ya utalii, ikiwemo utalii wa usiku na uwepo aina mbalimbali ya Wanyama kama vile makundi ya tembo wakubwa.
Hifadhi hiyo yenye mandhari ya asili yenye upekee, pamoja na uanzishaji wa mazao mapya ya utalii Mambo hayo yameifanya hifadhi hiyo iliyopo mkoani Manyara kuendelea kuwavutia wageni wengi zaidi hususani kuelekea mwishoni mwa mwaka na kuchangia ongezeko la mapato.
Ofisa Uhifadhi Daraja la Pili anayeshughulikia masuala ya utalii katika hifadhi hiyo, Calvin Lyakurwa, amesema kuwa utalii wa usiku unaendelea vizuri na umeanza kuvutia idadi kubwa ya watalii.
Kwa mujibu wa takwimu za hifadhi, kuanzia Oktoba Mosi hadi Desemba 15 mwaka huu, Tarangire imepokea wageni 73,372 na kuingiza mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 11.9, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya shilingi milioni 800 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Amesema nchi zinazoongoza kuleta watalii katika hifadhi hiyo ni Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, ikiwemo Ujerumani na Uingereza, huku utalii wa ndani nao ukiendelea kukua.
Kwa upande wake, muongoza watalii wa Kampuni ya Kilimanjaro Unforgettable, Laurent Samila, amesema kuanzishwa kwa utalii wa usiku kumeongeza fursa za ajira na kuimarisha shughuli za waongoza watalii.
#StarTvUpdate