
Maelfu ya raia walijitokeza kushiriki kwenye maandamano hayo makubwa wakipinga shinikizo la kuondolewa kwa waasi wa M23 katika mji wa Uvira. Kwa masaa kadhaa,shughuli zote za kila siku zilisimama katika mji wa Goma, huku maduka na masoko vikiwa vimefungwa. Mama huyu aliyeshiriki kwenye maandamano hayo lakini anaeleza hisia zake.
“wamefika kwangu nyumbani na kuniambia kwamba kuna maandamano, tumepewa makaratasi yenye ujumbe mbalimbali na hivyo tumelazimika kwenda kushiriki badala ya kuwatafutia watato wetu chakula. Kwa hiyo tumeona ni vizuri kwenda kwenye maandamano hayo ili kutafuta suluhisho.”
Wananchi hawa, miongoni mwao wakiwa wale kutoka katika miungano mbalimbali ya kiraia, walipata fursa ya kusoma malalamiko yao mbele ya ofisi kuu ya kikosi cha walinda amani wa Umoja wa mataifa nchini kongo, Monusco wakisisitiza umuhimu wa usalama na ulinzi katika eneo hilo.
Ikumbukwe kuwa mwanzoni mwa wiki iliyopita, waasi wa M23 walitangaza nia yao ya kujiondoa kutoka kwenye mji huo wa kimkakati kufuatia ombi la Marekani lililotaka waondoke mara moja.