Ripoti zilizotolewa na idara ya ujasusi wa Marekani zimeonya kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin bado hajaacha malengo yake ya kuyateka maeneo yote ya Ukraine na kurejesha sehemu za ardhi ya Ulaya ambazo awali zilikuwa chini ya himaya ya Umoja wa Kisovieti, huku baadhi ya sehemu hizo zikiwa zinapatikana ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Urusi imepuuzilia mbali ripoti hizo ikisema haifahamu ikiwa vyanzo vilivyotajwa na Shirika la habari la Reuters ni vya kuaminika, lakini ikasisitiza kuwa ripoti hiyo si sahihi, Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amesema wameona ripoti kadhaa kuhusu hilo huku akitilia mashaka usahihi wake.
” Hii ni katika hali ambayo idara za ujasusi hujikuta kuwa na fikra, utafiti na hitimisho potofu. Hili si kweli hata kidogo, ” alisisitiza Peskov.
Ripoti hizo zilizotolewa na vyanzo sita huku moja ya ripoti ikiwa ilitolewa mwishoni mwa mwezi Septemba, zinatoa picha tofauti kabisa na inayoelezwa na Rais wa Marekani Donald Trump na wapatanishi wake wa amani katika mzozo huu wa Ukraine, ambao wamekuwa wakinadi kuwa Putin ana dhamira ya kuumaliza mzozo huo na zinakinzana na kauli ya hivi majuzi iliyotolewa na Putin kuwa hana nia ya kuishambulia Ulaya na kuwa yeye si tishio kwa bara hilo.
Jenerali wa Jeshi la Urusi auawa mjini Moscow
Jenerali mmoja wa jeshi la Urusi ameuawa siku ya Jumatatu mjini Moscow baada ya gari lake lililotegwa bomu kuripuka. Jenerali huyo aliyeuawa alikuwa Mkuu wa Kurugenzi ya Mafunzo ya Uendeshaji kwenye Jeshi la Urusi na amefahamika kama Luteni Jenerali Fanil Sarvarov . Msemaji wa Kamati ya Uchunguzi ya Urusi Svetlana Patrenko amesema Jenereli Sarvarov amefariki kutokana na majeraha aliyoyapata na kwamba tayari uchunguzi umeanzishwa huku akisisitiza kuwa moja ya sababu za mauaji hayo ni uhusika wa idara ya Ujasusi ya Ukraine.
Taarifa kutoka Urusi zimeripoti kuwa gari hilo liliripuka Jumatatu majira ya saa moja asubuhi, likiwa kwenye maegesho ya magari katika mtaa wa Yaseneva kusini mwa mji wa Moscow huku dereva wa Jenerali huyo akiwa ndani ya gari lililoripuka. Serikali ya Ukraine haijazungumza chochote juu tukio hili, licha ya Urusi kuishutumu kuhusika. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Rais Vladimir Putin amearifiwa mara moja kuhusu mauaji ya Sarvarov ambaye alitajwa na Wizara ya Ulinzi kuwa aliwahi kupigana vita vya Chechnya na kushiriki katika operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Syria.
Haya ni mauaji ya tatu ya aina hii katika kipindi cha mwaka mmoja ambayo yanawalenga maafisa wakuu wa jeshi la Urusi, huku Kiev ikiwa ilitangaza kuhusika katika baadhi ya mashambulizi hayo tangu Ukraine ilipovamiwa na Urusi . Desemba mwaka 2024, idara za usalama za Ukraine zilidai kufanya shambulizi kama hili dhidi ya mkuu wa vikosi vya atomiki vya Urusi Luteni Kanali Igor Kirillov, aliyeuawa kwa bomu lililotegwa kwenye pikipiki nje ya makazi yake.
(Vyanzo: Reuters, AP)