SERIKALI ya Kenya imesema kuwa imefanikiwa kuwaokoa raia wake 119 waliokuwa wamekwama nchini Myanmar. Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Kigeni, Katibu anayesimamia masuala ya raia wanaoishi ughaibuni amesema kuwa operesheni hiyo ilifanikishwa kwa ushirikiano na mamlaka za Myanmar, baada ya kubaini vituo vilivyokuwa vikiwasajili watu kinyume cha sheria.
Vituo hivyo vipo katika maeneo ya jimbo la Karen, karibu na mpaka wa Myanmar na Thailand. Inaripotiwa kuwa vilikuwa vikitumiwa na makundi ya kihalifu kutekeleza ulaghai wa mtandaoni na kuwasajili watu kwa kazi zisizo halali.
Mamlaka za Myanmar zilitekeleza operesheni ya kuvamia vituo hivyo, kuwakamata baadhi ya washukiwa, pamoja na kuharibu miundombinu ya vituo hivyo. Operesheni hiyo, iliyofanyika mwezi Septemba 2025, ilisababisha mvutano kati ya serikali na makundi ya waasi yanayodhibiti maeneo kadhaa nchini humo. SOMA: RC Makalla akutana na Balozi Mdogo wa Kenya
Takribani Wakenya 200 walitafuta hifadhi katika kambi za kijeshi za Myawaddy na Shwe Kokko, huku wengine 100 wakivuka mpaka na kukimbilia nchini Thailand kwa ajili ya usalama wao. Ingawa jumla ya Wakenya 126 waliokolewa, ni 119 pekee ambao tayari wamerejeshwa nchini Kenya. Wengine saba wanatarajiwa kurejea hivi karibuni kutokana na mabadiliko ya tiketi zao za usafiri.
Serikali ya Kenya imeeleza kuwa bado kuna Wakenya 198 wanaosubiri kurejeshwa nchini, wakiwemo 66 walioko Thailand na 129 walioko Myanmar. Aidha, Wakenya wengine 86 bado wanapatiwa hifadhi katika kambi za kijeshi. Kwa mujibu wa serikali, wengi wa waliokumbwa na hali hiyo waliingia Thailand kwa kutumia viza za utalii, kisha kuhusika katika shughuli za ajira bila kufuata sheria za kazi za nchi hiyo.
