Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohamed Janabi amezitaka nchi za Afrika kuongeza fedha katika bajeti zao za afya, ili kupambana na kupungua kwa misaada ya rasilimali fedha.

Amesema hiyo imetokana na kujitoa kwa mataifa makubwa ikiwemo Marekani, hali iliyosababisha kupungua kwa asilimia 70 ya rasilimali fedha.

Profesa Janabi ameyasema hayo leo Desemba 22, 2025 wakati WHO kupitia Ofisi yake ya Kanda ya Afrika (WHO-AFRO) ilipokuwa ikisaini Hati ya Makubaliano (MoU), kuimarisha ushirikiano wa kikanda wa afya na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) katika Ofisi za WHO Tanzania.

Amesema asilimia kubwa ya milipuko inatokea katika nchi za Afrika, na katika kuishughulikia inahitaji rasilimali fedha nyingi, lakini mdau mkubwa aliyefadhili amejitoa, hivyo kupunguza misaada kwa kiwango kikubwa.

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohamed Janabi akizungumza baada ya kusaini MoU na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), katika Ofisi za WHO Tanzania leo Jumatatu Desemba 22, 2025.

“Misaada imepungua kwa asilimia 70, kilichobaki sasa nchi zinatakiwa kujipanga upya katika kujisaidia kwa kutenga bajeti kubwa za afya ili kuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto hizi pindi zinapojitokeza,” amesema.

Amesema kupungua kwa misaada hiyo pia ilichangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa rasilimali watu kwa asilimia 25, na hivyo wataalamu wengi wenye ujuzi mkubwa waliondoka.

“Tulipambana na Ebola ambayo tulitumia siku 90 kuidhibiti na wakati tunakabiliana nayo ilikuwa sehemu ya mbali ambayo ilitulazimu kusafiri kwa siku tano kufika, lakini tulifanikiwa kupeleka shehena za dawa na mahitaji maalumu na tulianza kutoa huduma kwa jenereta na sasa tumefanikiwa kupeleka sola,” amesema.

Profesa Janabi pia amesema magonjwa ya kuhara ni changamoto kubwa inayoibuka kwa sasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Karibu nchi 15 zimepata magonjwa ya milipuko ikiwemo polio Afrika magharibi, Ethiopia wamepata Marburg lakini zote tumefanikiwa kudhibiti,” amesema.

Amesema mabadiliko ya tabianchi hayaji na changamoto ya magonjwa pekee, kwani yamekuja na suala la usalama wa chakula pia.

Aidha amesema katika nchi mbalimbali magonjwa yasiyoambukiza imekuwa ni changamoto barani Afrika asilimia 32 ya watu wana uzito uliokithiri, hali aliyoitaja kuwa ni hatari kwa afya hapo baadaye.

Pamoja na hayo, Profesa Janabi amesema utengwaji wa fedha katika bajeti ya afya utasaidia pia kushughulikia afya ya vijana balehe,

“Afrika ina idadi kubwa ya vijana wadogo, linaweza kuwa kundi litakaloleta changamoto miaka ya mbele inabidi tuwatayarishe. Sisi wadau wa afya tunalitazama kwa ukubwa sana hili kundi,” amesema.

Licha ya kutenga rasilimali fedha za kutosha, Profesa Janabi amezitaka nchi za Afrika kuamka na kuona namna zinavyoweza kuanza uzalishaji na kuacha kutegemea asilimia 80 ya dawa na asilimia 99 ya chanjo, kutoka nje ya bara hilo.

“Nchi zinazotaka kuanzisha viwanda sisi tunazisaidia, lazima   wenyewe tuzalishe dawa tuondoke kwenye utegemezi, gharama yake ni kubwa lazima tujitegemee, hivyo tunahimiza nchi zote 47 ziweze kujitegemea kifedha,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe (wa kwanza kushoto) akizungumza baada ya kusaini MoU na WHO katika Ofisi za WHO Tanzania leo Jumatatu Desemba 22, 2025.

Akihitimisha hotuba yake, Profesa Janabi amewahamasisha Watanzania wajitokeze kuomba kazi katika nafasi za juu WHO.

WHO (AFRO) na ECSA-HC zimesaini MoU,  yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuboresha matokeo ya afya na kujenga mifumo thabiti katika eneo la Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

MoU hii inaweka mfumo rasmi wa ushirikiano unaoendana na Mpango wa Kazi wa Jumla wa 14 wa WHO (GPW 14) pamoja na vipaumbele vya kikanda, na kuimarisha juhudi za pamoja za kuharakisha maendeleo kuelekea bima ya afya kwa wote, usalama wa afya na kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Profesa Janabi, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto tata za afya.

“MoU hii si tu kuhusu ushirikiano kati ya taasisi, bali muhimu zaidi, ni kuhusu kutoa matokeo bora ya afya kwa Waafrika, hususani makundi yaliyo hatarini, katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini,” amesema.

Kupitia ushirikiano huu, WHO AFRO na ECSA-HC zitashirikiana katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, yakiwemo uimarishaji wa huduma za afya ya msingi, kinga na udhibiti wa magonjwa, maendeleo ya rasilimali watu katika sekta ya afya, mabadiliko ya afya ya kidijitali, ulinganifu wa kanuni na mifumo ya udhibiti, utafiti na ubunifu, pamoja na kuimarisha utayari na mwitikio dhidi ya dharura za afya ya umma.

Makubaliano hayo pia yanasisitiza umuhimu wa mbinu za kikanda katika kukabiliana na vitisho vinavyoibuka kama vile mabadiliko ya tabianchi, usugu wa vimelea dhidi ya dawa na milipuko ya magonjwa ya baadaye.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe ameeleza umuhimu wa makubaliano hayo katika kuziunga mkono nchi wanachama.

“MoU hii inaimarisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na WHO AFRO na kuongeza uwezo wetu wa pamoja wa kuisaidia nchi kujenga mifumo ya afya iliyo imara, yenye usawa na inayomlenga mwananchi. Kwa pamoja, tutaendeleza suluhu za kikanda zitakazojibu vipaumbele na changamoto za afya zinazofanana,” amesema.

“Kuna changamoto ya magonjwa ya mlipuko na magonjwa mengine kwa sasa asilimia 37 ya vifo vinatoka na magonjwa yasiyoambukiza. Mabadiliko ya tabianchi na usugu wa vimelea vya dawa ndiyo changamoto kubwa zaidi barani Afrika, hivyo tumeungana pamoja kuona namna tutakavyoshirikiana,” amesema.

Dk Kapologwe amesema jumuiya ya sasa inahitaji sana ushirikiano ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na changamoto zilizopo ikiwemo upatikanaji fedha, ikilinganishwa na idadi ya watu iliyokua takribani bilioni 1.3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *