
Vikosi vya Syrian Democratic Forces (SDF) vimeonesha kutokuwa na nia ya kupiga hatua katika mazungumzo ya kujumuishwa na serikali ya Syria, waziri wa mambo ya nje wa nchi jirani ya Uturuki alisema Jumatatu.
“Tunaona kuwa SDF hawana nia njema ya kupiga hatua katika mazungumzo kuhusu kujumuishwa na serikali ya Syria,” Hakan Fidan alisema katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad Hassan al-Shaibani mjini Damascus, mji mkuu wa Syria, baada ya mkutano wao.
Aliongeza kuwa tabia ya kundi hilo imekuwa kikwazo kikubwa katika mazungumzo yanayoendelea, akilishtumu kwa kuratibu baadhi ya shughuli zake na Israel.
“Ukweli ni kuwa SDF inafanya baadhi ya shughuli zake kwa kushirikiana na Israel kwa sasa na hii inasababisha kikwazo kikubwa kwa majadiliano yanayofanyika na serikali ya Syria,” alisema.
Waziri huyo wa mambo ya nje alifanya mazungumzo mapana, kwanza kuhusu ushirikiano wa mataifa yao mawili, akieleza kuwa walizungumzia usalama katika kanda na tishio kwa uthabiti wa Syria.
Kauli hiyo imejiri huku Fidan, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Yasar Guler, na mkuu wa usalama wa taifa wa Uturuki Ibrahim Kalin wakiwa katika ziara ya kikazi mjini Damascus.
Ujumbe huo unatarajiwa kukutana na Rais wa Syria Ahmad al-Sharaa na magisa wengine wa ngazi za juu ili kutathmini kwa kina uhusiano wa Uturuki na Syria katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kufuatia kupinduliwa kwa utawala wa Bashar Assad.